ZILE kelele za kabla ya kuanza kupigwa kwa mechi za makundi ya michuano ya CAF zimeisha baada ya matokeo yasiyotarajiwa kwa klabu nne za Tanzania – mbili zikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine kama hizo zikikiwasha Kombe la Shirikisho.
Yanga na Simba zilizopo Ligi ya Mabingwa zenyewe zilianza mechi zikiwa nyumbani na kila moja kupata matokeo yasiyotarajiwa, wakati wageni wa hatua ya makundi zikicheza Kombe la Shirikisho, Azam FC na Singida Black Stars kila moja ikichapika kwa mabao 2-0 ugenini.
Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja kupitia Prince Dube aliyeizamisha AS Far Rabat ya Morocco, wakati Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikilala 1-0 mbele ya Petro de Luanda ya Angola.
Kwa upande wa Azam na Singida kila moja ililala kwa mabao 2-0, Wanalambamba wakipigwa na AS Union Maniema ya DR Congo, wakati wauza wlizeti wakifumuliwa na CR Belouizdad ya Algeria licha ya kila moja kuonyesha upinzani licha ya ugeni katika michuano hiyo.
Kwa sasa timu hizo nne za Tanzania zinabadilishana kwa mechi za raundi ya pili ya makundi, Simba na Yanga zikienda ugenini wakati Azam na Singida zinarudi nyumbani ili kujiuliza upya kabla ya michuano hiyo kusimama hadi Januari, mwakani ili kupisha fainali za Afcon 2025.
Hapa chini ni uchambuzi wa mechi zilizocheza timu hizo za Tanzania na mitihani zinayokabiliana nayo kwa mechi zijazo ili kujitengenezea nafasi ya kujaribu kupenya kwenda robo fainali kupitia makundi ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
YANGA FRESHI
Yanga ilianza kampeni hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ngumu ya AS FAR Rabat kwenye mchezo ambao ilionekana kama bingwa huyo wa kihistoria wa soka nchini angekwenda kukwama mbele ya Waarabu hao.
Pengine kubezwa huko kuliibeba Yanga, ambapo ilijipanga sawasawa kukabiliana na Waarabu hao ikitawala vizuri mchezo na kupata ushindi huo muhimu ambao sasa unaifanya kushika nafasi ya pili kwenye kundi lao B linaloongozwa na Al Ahly wote wakiwa na pointi sawa wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, Yanga ushindi huo hautakiwi kuwafanya wabweteke kwani bado uhalisia ni kwamba kundi lao ni gumu kutokana na ubora wa timu ambazo imepangwa nazo zikiwemo Ahly, JS Kabylie na FAR Rabat.
Ushindi ambao Yanga imeupata unatakiwa kuwajenga kisaikolojia wachezaji wakati wanaifuata JS Kabylie wataochjeza nao Novemba 28 kwenye uwanja wa Hocine Ait Ahmed uliopo Kaskazini mwa mji wa Tuzi Ouzou, mji mkubwa wa pili kwa ukubwa nchini humo.
Yanga inatakiwa kuimarika wakati inaifuata Kabylie ambayo itakuwa na hasira za kutaka kubadilisha matokeo ikitoka kupoteza ugenini, ambapo kikosi cha kocha Pedro Goncalves kina kazi ya kuhakikisha kinatumia nafasi zaidi na kutoruhusu wenyeji kuwatangulia kwa bao la mapema.
SIMBA YATIBUA
Simba imetibua rekodi ya mechi za nyumbani baada ya juzi kulala kwa bao 1-0 mbele ya Petro Atletico huku Wekundu hao wakionekana na upungufu flani kikosini.
Kipigo cha juzi ni cha kwanza kwa Simba tangu ilipofumuliwa mabao 3-0 na Raja Casablanca katika mechi za makundi iliyopigwa Kwa Mkapa Februari 18, 2023, lakini ikitimiza mechi ya nne mfululizo bila kupata ushindi nyumbani tangu ilipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Zanzibar, Simba ililazimishwa sare ya 1-1 na RS Berkane ya Morocco, kisha ikatoka sare na Gaborone United ya Botswana na suluhu dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya eSwatini kabla ya juzi kulala 1-0 kwa Petro ya Angola.
Lawama kubwa kwa Simba zinakwenda kwenye makundi mawili ambapo kwanza ni wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi ambazo imezitengeneza ambazo kama ingezitumia matokeo hayo yangekuwa ngumu kutokea.
Kundi la pili la lawama hizo zitakwenda kwa kocha Dimitar Pantev ambaye amekosolewa kwa namna alivyopanga kikosi akicheza kwa dakika 52 bila mshambuliaji halisi na kuifanya timu hiyo kuteseka kwenye eneo la mwisho. Simba kupoteza wakati Esperance de Tuinis zikitoka sare nyumbani kumezifanya kuwa timu pekee ambazo hazikufanikiwa kushinda nyumbani zote zikiwa kundi moja la D huku zingine sita zikishinda vizuri.
Simba bado haijatoka kwenye mstari licha ya kupoteza mchezo huo, lakini kuna mambo lazima ibadilike kwanza ni namna ya kupanga kikosi na pia itatakiwa kuwajua vyema Stade Malien ambao waliilazimisha sare Esperance, Waarabu hao wakiwa nyumbani.
Historia inaonyesha Simba imewahi kupoteza mechi mbili na bado ikaenda kufuzu robo fainali, na sasa inatakiwa kujipanga na kwenda kubadilisha matokeo hayo mbele ya Stade Malien ingawa hautakuwa mchezo rahisi kutokana na nidhamu ya wachezaji wa timu hiyo pinzani.
Hata hivyo, kama Simba itaamua kujipanga vyema kwa mechi ya Malien inaweza kuweka sawa hesabu kwa mechi zilizosalia katika Kundi D ili kutoboa kwenda robo fainali kwa mara nyingine.
AZAM FC
Azam FC inayoshiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya michuano ya CAF ilianza na mguu mbaya michuano hiyo kwa kupoteza kwa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Union Maniema ya DR Congo katika mechi ambao matajiri hao wa Chamazi watajilaumu kutoimaliza mapema.
Pengine ni ugeni wa timu hiyo kwani huo ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC wa hatua ya makundi tangu klabu hiyo ianzishwe, ikionekana kama ilipata presha kubwa ya kukosa utulivu wa kutengeneza matokeo mazuri mbele ya Wakongomani hao.
Mshambuliaji wa Azam, Japheth Kitambala kila atakapokuwa anakumbuka nafasi alizopoteza kuwafunga waajiri wake wa zamani atakuwa anakosa raha kwani ziliichongea timu yake kukosa ushindi.
Straika huyo aliyetua Azam msimu huu akitokea Union Maniema alikosa mabao mawili ya wazi kipindi cha kwanza kabla ya kurudia kipindi cha pili wakati wenyeji wakiwa wanaongoza kwa bao moja kisha kuongeza jingine lililoifanya timu hiyo kufuata nyayo za Namungo na Singida BS kuanza mechi za kwanza za makundi na vipigo.
Namungo ilikuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kucheza makundi ya CAF 2020 na kuweka rekodi mbaya ya kupoteza mechi zote sita bila kufunga bao hata moja. Kwa upande Singida ilianza mapema Jumamosi kucharazwa 2-0 na CR Belouizdad ikiwa ugenini.
Mbali na makosa ya safu ya ushambuliaji pia eneo la ulinzi lilikosa utulivu, likafanya makosa ambayo yaliipa Maniema mabao mawili.
Azam baada ya matokeo hayo inarudi nyumbani itakapokuwa mwenyeji wa Wydad Athletic ya Morocco Novemba 28 katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar ambapo Waarabu hao wakitoka kushinda kwenye mchezo wa kwanza walioshinda nyumbani kwa mabao 3-0 dhidi ya Nairobi City.
Azam inatakiwa kutembea na falsafa za Yanga kwamba kila kitu kinawezekana kama itajipanga kwani licha ya Wydad kuwa na kikosi imara, lakini jeshi la kocha Florent Ibenge linaweza kujipanga na kubadilisha mambo. Kitu ambacho Azam inatakiwa kujipanga ni kuimarisha safu yake ya ulinzi kwani Waarabu hao wana safu nzuri ya ushambuliaji na pia eneo la ushambuliaji linatakiwa kuwa katili kumalizia vyema nafasi watakazotengeneza.
SINGIDA BLACK STARS
Singida Black Stars ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria inayofundishw ana kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic.
Licha ya Singida kupoteza ikiwa ni mechi ya kwanza ya kihistoria hatua ya makundi, lakini kikosi hicho cha kocha Miguel Gamondi hakikucheza vibaya kilipambana kuonyesha mipango na kutengeneza nafasi. Kama ilivyokuwa Azam Singida inarudi kujiuliza itakapokutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo ilitangulia kushinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya AS Otoho kutoka Kongo Brazaville mchezo utakaopigwa Novemba 30 Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Singida ni mpya kwenye mashindano hayo, lakini ina kikosi chenye wachezaji wazoefu ambao wameshiriki mechi kama hizo huku ikiwa na kocha anayejua kutafuta ushindi. Baada ya kumkosa kiungo mkongwe Khalid Aucho, kwenye mchezo ujao atakuwepo, lakini muhimu ni namna safu ya ushambuliaji italazimisha Stellenbosch kufanya makosa kisha iyatumie.Kwa namna Kundi C lilivyo Singida inapaswa kushinda mechi ijayo kabla ya kusubiri kukabiliana na AS Otoho ya Kongo Brazzaville ‘back to back’ mwakani kuamua hatima ya kutinga robo fainali.
The post HUKO CAF WIKI HII…NI YANGA TU…..HAKUNA CHA SIMBA WALA UBAYA UBWELA😂😂😂…… appeared first on Soka La Bongo.



