KULIKUWA na siku mbaya kazini Simba juzi. Ilipogonga saa 12 kamili jioni mashabiki wao hawakuamini walichokiona kwa macho yao.
Kuanzia wale ambao walikuwa uwanjani katika majukwaa mbalimbali hadi waliokuwa wanafuatilia pambano dhidi ya Petro de Luanda wakiwa majumbani na katika sehemu za starehe.
Mnyama aliondoka uwanjani akiwa ameloa bao moja na kuivuruga kabisa ile kauli yao maarufu ya michuano ya CAF ‘Kwa Mkapa Hatoki Mtu’. Petro waliondoka zao uwanjani salama. Wakafika hotelini wakaoga, wakala chakula cha usiku na baadaye wakaenda zao uwanja wa ndege kurudi nyumbani.
Nyuma yake waliacha vikundi vya mashabiki vikiwa nje ya uwanja vikilaumu kila kitu. hata mitandaoni mashabiki walilaumu kila kitu.
Tuanzie wapi? Tuanzie kwa namna ambavyo kocha Dimitr Pantev alivyopanga kikosi chake.
Kuna hadi mashabiki wanataka aondoke kikosini kwa sababu alikipanga kikosi chake bila ya kumuanzisha mshambuliaji yeyote yule uwanjani.
Suleiman Mwalimu, Jonathan Sowah na Steven Mukwala walikuwa wanatazama mpira kama sisi mashabiki. Walikuwa nje.
Pentev alijaribu kujifanya kwamba yupo mbele ya muda na akamuiga Pep Guardiola ambaye kuna wakati huwa anafanya hivyo. Anamtumia kiungo mmoja acheze kama mshambuliaji feki pale mbele. Kuna wakati akiwa na Barcelona alikuwa anamweka nje David Villa na kumpanga
Cesc Fabregas kama mshambuliaji wa kati ambaye pia ana jukumu kubwa la kucheza eneo la kiungo.
Pentev alifanya majaribio yake katika mechi ngumu akiwa kocha anayekaa katika benchi la mashabiki wenye vichwa vigumu. Iwe Simba au kwa watani wao Yanga, hakuna shabiki anayeweza kukubali timu ianze bila ya mshambuliaji.
Kitu pekee ambacho kinaweza kukuokoa ni mabao. Ni kweli sisi wengine tunamuelewa kwamba unapofanya hivyo unakuwa na lengo la kudhibiti eneo la kiungo lakini pia kitu muhimu kinakuwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na yeyote uwanjani anaweza kufunga.
Tatizo katika mfumo huu waliomuangusha Pentev ni Ellie Mpanzu na Morice Abraham. Kelele zote za kumtukana kocha na kutaka aondoke klabuni ni kwa sababu tu Mpanzu na Maurice walikosa mabao mawili ya wazi katika namna ya kushangaza.
Kama Mpanzu na Morice wangetumia nafasi zao leo Simba ingekuwa imeshinda 2-1 na tusingesikia kelele za mashabiki. Zaidi ni kwamba Pentev angeonekana kuwa ‘genius’ kwa namna ambavyo alianzisha kikosi chake bila ya mshambuliaji na bado akashinda mechi.
Mpanzu alimzunguka kipa wa Petro vizuri tu akabakia na nyavu lakini akakosa bao. Wanaomtetea wanadai kwamba ni kwa sababu alikosa balansi wakati akigeuka. Ukweli ni kwamba hakuna makini. Angetua zaidi angefunga. Kuna wachezaji wengi tu wanafunga vizuri tu pale. Kina Meddie Kagere walikuwa wanafunga mabao yale.
Matokeo yake Mpanzu amezua jambo jingine. Nje ya uwanja mashabiki wameanza kumchoka. Kuna hisia zimeanza kuja mbaya kwamba huenda hachezi kwa moyo katika jezi yao. Mpanzu anataka kuturudisha kule kule kwa kina Clatous Chota Chama na Aishi Manula ambao kwa muda mrefu walikuwa wako Simba lakini walikuwa wanaonekana wanahujumu.
Kitu kilichochekesha zaidi ni kwamba Mpanzu pia aliamsha hisia za mashabiki kwamba uwanja wa taifa ‘umechezewa’ na watani zao Yanga kisha wakaamua kukimbilia zao Unguja kucheza mechi zao za CAF kwenye Uwanja wa Amaan.
Sijui kama umenielewa vizuri neno ‘kuchezewa’, lakini katika lugha ya mpira wanaamini kwamba uwanja umefanyiwa mambo ya kishirikina ili Simba wasifanye vema. Siamini katika jambo hili. Siamini katika imani ya uwanja au siku ya kucheza mechi. Naamini katika timu nzuri na yenye wachezaji makini.
Haya maneno ameyaleta Mpanzu lakini wakati ule Simba ikinyanyasa wakubwa katika uwanja wa Mkapa hakukuwa na ishara za mambo ya nuksi katika uwanja. Sana sana kulikuwa na kauli ya kwamba ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’.
Haya mambo huwa yanaletwa zaidi na viwango vya timu na wachezaji. Huyu Mpanzu amekuwa hivi tangu msimu uanze na haishangazi kuona amekosa bao lile. Kila nikimtazama namuona anacheza kama vile analazimishwa. Sura yake haina furaha. Sijui ni kitu gani kinamkabili.
Na sasa maisha yataendelea vipi Simba? Kwanza kabisa nina imani na Pentev. Nashangaa mashabiki wamegeuka ghafla wakati wote walikubaliana kwamba alikuwa ni kocha mwafaka kufundisha Simba
Baada ya kuiona timu yake ya zamani Gaborone United ilivyoisumbua Simba katika mechi za kufuzu kuelekea hapo.
Kwa ubora wa wachezaji wa Simba, kama Pentev akifanikiwa kuingiza alichonacho katika miili yao na wakacheza asilimia 80 tu kama ambavyo Gaborone United ilicheza na Simba licha ya kutolewa, basi Simba watakuwa wameipata timu ya maana.
Vipi kuhusu kundi? Mambo bado. Kuna imani kwamba timu za Tanzania zinatakiwa kushinda mechi zake tatu za nyumbani kwa ajili ya kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali. Ni kweli katika mpira wa Afrika jambo hili ni muhimu lakini katika miaka ya karibuni timu zetu zimebadilika kwa kiasi kikubwa.
Wakubwa hawa, hasa Simba na Yanga wanaweza kushinda mechi yoyote ya soka ugenini katika siku za karibuni. Ni mapema kuikatia Simba tamaa ila wanachopaswa kufanya ni kuhakikisha wanafidia pointi hizi kwa kujaribu kwenda kuchukua pointi tatu au moja wakiwa ugenini.
Ni katika mechi yao ijayo dhidi ya Stade Mallen au Esperance du Tunis au watakaporudiana na Petro.
Isionekana kwamba nguzo kubwa ya kushinda ni pale timu inapocheza mechi za nyumbani tu. unaweza kucheza ugenini ukapata sare mbili au kushinda mechi moja na kisha ukarudi nyumbani kufanya kazi nzuri ya kuchukua pointi sita.
Kuhusu kocha sijui akili za mabosi wao zitakuwa vipi. Naelewa kwamba mashabiki wamepatwa na mihemko na wanataka mabosi wao wafuate njia za watani. Mtani alifungwa kule Malawi akaamua kumfukuza Roman Folz kule kule.
Nadhani mashabiki wanatamani kuona viongozi wao wanafuata njia ile ile lakini kila nikikumbuka namna Gaborone United walivyokuwa wanacheza natamani kuona mabosi wa Simba wakimpa muda Pentev.
Sioni kama Simba wanacheza vibaya sana na kama ukiniuliza kwanini hawakushinda juzi basi moja kwa moja nitapeleka zaidi lawama zangu kwa upotevu wa nafasi.
Na bahati mbaya zaidi kwa Simba ni kwamba hata bao lililofungwa lilitokana na mpira ulioguswa na beki wa kati wa Simba na kumpoteza maboya Yakoub Suleiman. Tayari mpira alikuwa ameshauona na alikuwa amepanga kuuokoa lakini ukapoteza mwelekeo.
Makala haya yameandikwa na EDO Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye gazeti la MwanaSpoti.
The post EDO KUMWEMBE: PENTEV ALITAKA KUJIFANYA GUARDIOLA…MPANZU KAMA CHAMA TU….. appeared first on Soka La Bongo.


