PARIS: KOCHA wa Tottenham Hotspur Thomas Frank ameapa kusimama imara na mpango wake wa ujenzi wa muda mrefu wa kikosi chake licha ya kupokea kipigo Kizito cha mabao 4-1 kutoka kwa Arsenal kwenye Premier League wikiendi iliopita, wakati timu huu yake ikijiandaa kwa mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris St Germain usiku wa leo Jumatano.
Tottenham walicharazwa vibaya na mahasimu wao wa Kaskazini mwa London washika mitutu Arsenal, huku Eberechi Eze akifunga mabao matatu (Hattrick) katika mchezo huo mkubwa wa Jumapili.
Kikosi cha Frank kimeshinda mechi moja pekee kati ya tano za mwisho za EPL, hali inayoongeza shinikizo kwa kocha huyo wa Kidenmark aliyeteuliwa mwezi Juni kuchukua nafasi ya Ange Postecoglou aliyefutwa kazi.
Baada ya kupata ushindi kwenye mechi tano katika 12 zilizopita, Tottenham wanashika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 18, 11 nyuma ya vinara Arsenal lakini Frank alisema anaamini katika uwezo wake wa kuibadilisha timu hiyo.

“Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho asilimia elfu ni kwamba najua jinsi ya kujenga timu na klabu. Tutafanya hivyo. Sehemu ya kukubali kazi hii ni pamoja na kukabiliana na changamoto. Ni sehemu ya kusimamia vikwazo, kujifunza na kusonga mbele.” – Frank aliwaambia waandishi wa Habari jijini Paris.
Frank, ambaye ni kocha wa tano wa kudumu wa Tottenham katika kipindi cha miaka sita, anaelekeza sasa nguvu zake kwa mabingwa wa Ulaya PSG na kusema kuwa kikosi chake kina uwezo wa kujibu mapigo.
“Sasa tutakabiliana na moja ya timu bora zaidi Ulaya, ugenini, Hivyo ni changamoto nzuri ambayo tuko tayari kwa asilimia mia moja, na ninaamini tutarejea na matokeo mazuri.” – amesema kocha huyo mwenye umri wa miaka 52.
Tottenham wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupata ushindi katika michezo miwili kati ya minne, na ushindi Paris unaweza kuwapa nafasi ya kuingia kwenye kumi bora.
The post Thomas Frank atamani ‘pointi’ za PSG first appeared on SpotiLEO.








