DAR ES SALAAM: MWANARIADHA wa Kimataifa wa Tanzania kutoka timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Alphonce Simbu, ameenda nchini Ufaransa ambako anatarajiwa kushiriki sherehe za Tuzo za Wanariadha Bora wa Dunia 2025 zinazoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Dunia (World Athletics).
Hafla hiyo itakayofanyika Novemba 30, 2025 jijini Monaco, itawakutanisha wanariadha 12 bora kutoka mataifa mbalimbali ambao wamefanikiwa kuingia kwenye hatua ya mwisho ya mchakato wa tuzo hizo. Simbu ni miongoni mwa watakaowania tuzo hizo katika vipengele tofauti.
Nyota huyo wa mbio ndefu (marathoni) anawania tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mbio za Nje ya Uwanja kwa Wanaume, akipambana na mpinzani wake wa mwisho, Sebastian Sawe kutoka Kenya, baada ya wote wawili kupenya kwenye mchujo mkali uliowahusisha wanariadha wa viwango mbalimbali duniani.
Akizungumza kabla ya safari yake, Simbu alimshukuru Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, Serikali, Watanzania, wadau wa michezo na vyombo vya habari kwa sapoti yao ambayo amesema imekuwa nguzo kubwa katika mafanikio yake.
“Mafanikio yangu yasingewezekana bila nguvu ya pamoja kutoka kwa viongozi, mashabiki na jamii ya michezo. Nawashukuru Watanzania kwa kura zao na sapoti yao ya muda mrefu,” alisema Simbu.
Aidha, alitoa shukrani maalum kwa Watanzania kwa kuendelea kumpigia kura katika kipengele cha Mwanariadha Bora wa Kiume wa Mbio za Nje, akibainisha kuwa anaelekea Monaco kwa matumaini makubwa kuelekea tuzo hizo.
Simbu ameahidi kuendelea kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kupigania mafanikio zaidi katika anga la riadha duniani.
The post Simbu aifuata tuzo Ufaransa first appeared on SpotiLEO.



