LONDON: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca, anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kutafuta mbadala wa kiungo wake muhimu, Moises Caicedo, kuelekea mchezo wa ligi kuu ya England (Premier League) dhidi ya Leeds United usiku wa leo Jumatano.
Caicedo, ambaye amecheza mechi 50 kati ya 51 tangu Maresca achukue timu hiyo, alioneshwa kadi nyekundu na kutolewa nje kwenye sare ya 1-1 dhidi ya vinara wa ligi Arsenal Jumapili iliyopita, hivyo ataikosa safari ya Elland Road.
Chelsea pia itaendelea kumkosa beki Levi Colwill, pamoja na viungo wa ulinzi Romeo Lavia na Dario Essugo, wote wakiwa majeruhi. Mshambuliaji Cole Palmer alikuwepoi kwenye benchi dhidi ya Arsenal baada ya kukosekana kwa muda mrefu. Maresca amesema timu haina budi kupata suluhu mpya bila wachezaji hao muhimu.

“Tukiwa na Cole, tukiwa na Moises, tukiwa na Levi timu inakuwa bora zaidi. Lakini wanapokosekana, tunatafuta njia mbadala. Tulifanya hivyo Levi alipokosekana, tulifanya hivyo Cole alipokuwa nje, na sasa tunahitajika kufanya kitu tofauti kwa sababu ya Moi.”
Kiungo kijana Andrey Santos anaonekana kuwa chaguo la moja kwa moja kuchukua nafasi ya Caicedo. Na Maresca anasema Andrey yuko tayari na nafasi yake ya asili ni namba sita, sawasawa na ya Caicedo.
Kocha huyo pia amesema anaweza kumtumia Reece James katika nafasi tofauti, huku kijana Josh Acheampong akitajwa kama chaguo jingine lenye uwezo wa kucheza katika eneo la kiungo wa ulinzi.
Kuhusu Palmer, Maresca ameeleza kuwa bado hawezi kucheza dakika 90. Akifichua kuwa anaweza kuanza kwa kupewa dakika chache taratibu hadi awe tayari kucheza mechi nzima.
The post Maresca ahaha kutafuta mbadala wa Caicedo first appeared on SpotiLEO.






