MANCHESTER: mashetani wekundu Manchester United wameshindwa kupanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo Ligi Kuu England baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na West Ham United katika mchezo wa Alhamisi usiku uliopigwa nyumbani kwao Old Trafford, matokeo ambayo yaliwaacha wageni wakiendelea kusota kwenye eneo la kushuka daraja.
Baada ya kipindi cha kwanza kisicho na mvuto, United walipata bao la kuongoza dakika ya 58 kupitia Diogo Dalot. Hata hivyo, West Ham walirejea mchezoni dakika saba kabla ya mechi kuisha kupitia Soungoutou Magassa, jambo lililosababisha mashabiki wa United kulalamika kwa sauti mwishoni mwa mchezo.

Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, hakuficha hisia zake. Hasira na kukata tamaa. Amesema kuwa kikosi chake kimekuwa hakina uthabiti msimu huu na kukosoa namna walivyocheza katika tukio lililosababisha bao la kusawazisha.
Amesema walijua upungufu wa wachezaji warefu na hatari ya mipira ya juu, lakini bado walipaswa kufanya vizuri zaidi katika kulinda uongozi wao.
“Tulipaswa kutulia baada ya bao la kwanza. Tumepoteza pointi mbili tena,” amesema Amorim.
United sasa wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi 22, huku West Ham wakibaki katika nafasi ya 18 wakiwa na pointi 12 mbili nyuma ya Leeds United waliopo juu ya mstari wa kushuka daraja.
The post United yakwama nafasi ya nane first appeared on SpotiLEO.







