ISTANBUL: WAENDESHA mashtaka jijini Istanbul wametoa hati za kukamatwa kwa makumi ya wachezaji na maofisa wa soka kufuatia kashfa ya upangaji na ushawishi wa matokeo kupitia michezo ya kubeti, ambayo imeitikisa nchi hiyo.
Katika misako ya alfajiri iliyofanywa mapema leo Ijumaa, wachezaji kadhaa kutoka klabu kongwe za Uturuki wamekamatwa, akiwemo Mert Hakan Yandaş wa Fenerbahçe na Metehan Baltacı wa mabingwa watetezi Galatasaray.
Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) lilitangaza mwezi Oktoba kuwa lilikuwa likichunguza zaidi ya waamuzi 150 walioko kwenye ligi za kitaaluma kwa tuhuma za kushiriki kwenye ‘betting’ kwenye mechi za soka. Uchunguzi huo baadaye ulipanuka na kuhusisha wachezaji, viongozi wa klabu, wachambuzi wa TV na wadau wengine wa mchezo.

Mwezi uliopita, zaidi ya wachezaji 100 wa kulipwa wakiwemo 25 wanaocheza ligi kuu walipigwa marufuku kwa muda wakati uchunguzi ukiendelea.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Istanbul imetoa waranti kwa watu 46, na tayari 35 wamekamatwa, akiwemo mwenyekiti wa Ankaraspor, makamu mwenyekiti wa Antalyaspor, na mwenyekiti wa zamani wa Adana Demirspor.
Kwa mujibu wa shirika la habari DHA, aliyekuwa mwamuzi na mchambuzi Ahmet Çakar pamoja na mwamuzi wa sasa Zorbay Küçük pia wamewekwa kizuizini.
Katika taarifa yao, waendesha mashtaka hao wamesema uchunguzi wao umebaini kuwa Baltacı aliwahi kuweka dau kwenye mechi za timu yake, huku Yandaş akidaiwa kutumia mtu mwingine kuweka dau kwa niaba yake.
The post Wachezaji Galatasaray, Fenerbahçe matatani kwa ‘kubeti’ first appeared on SpotiLEO.








