KOCHA wa Simba, Seleman Matola, ameonyesha wazi masikitiko yake kufuatia kushindwa kwa washambuliaji wake kutumia nafasi muhimu walizozipata katika kipindi cha kwanza cha mchezo wa Mzizima Derby dhidi ya Azam FC.
Matokeo ya kipute hicho yalikuwa pigo kwa Simba, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika dakika 45 za mwanzo, Simba ilionekana imara na iliongoza mchezo kwa kiwango cha juu, ikitengeneza nafasi kadhaa za wazi. Hata hivyo, changamoto iliyoonekana kuwa kubwa ni ukosefu wa umakini na utulivu mbele ya lango, hali iliyowanyima mabao ambayo yangewapa uongozi mapema.
Licha ya kutawala eneo la kiungo na kumiliki mpira, safu ya ushambuliaji ilionekana kusuasua. Washambuliaji wao, Jonathan Sowah, Selemani Mwalimu na Steven Mukwala, walipata nafasi ya kucheza katika vipindi tofauti vya mchezo,
Lakini bado hawakuweza kuonyesha makali yanayotarajiwa kutoka kwao. Ulegevu huo ulipelekea mashabiki na benchi la ufundi kutafuta majibu juu ya kinachoendelea kwenye safu hiyo muhimu.
Baada ya mchezo huo Matola amesema timu yake ilianza kwa kasi na kujiamini, lakini kilichowangusha ni maamuzi yasiyo sahihi katika eneo la hatari.
Ameeleza kuwa wachezaji wake walishindwa kutumia nafasi walizotengeneza kutokana na kukosa utulivu, jambo lililoondoa uwezekano wa kupata bao la mwanzo ambalo lingeweza kubadilisha mwelekeo mzima wa mchezo.
Kocha huyo ameongeza kuwa dakika 10 za mwisho za kipindi cha pili ndizo zilizoangusha mpango wao wote wa mchezo.
Simba ilipoteza muelekeo, ikaonekana kuchoka, makosa madogo yakaanza kujitokeza. Makosa hayo yaliwapa Azam FC nafasi ya kufunga mabao mawili muhimu, yaliyokata kabisa kasi na morali ya wachezaji wa Simba.
“Tulipoteza muelekeo dakika 10 za mwisho katika kipindi cha pili na kuruhusu bao 2-0. Haikuwa bahati kwetu na tunajipanga kwa mchezo ujao,” amesema Matola, akiashiria umuhimu wa kufanya maboresho ya haraka katika eneo la ushambuliaji.
Kwa upande wa pili, Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, alikiri kuwa hawakuanza mchezo vizuri. Alibaini mapungufu hayo, alifanya marekebisho muhimu kipindi cha pili ambayo yalibadilisha mchezo kabisa. Mbinu alizozibadilisha ziliwapa nguvu mpya, na kikosi chake kikaanza kushambulia kwa ufanisi zaidi.
Ibenge alisema ushindi huo wa pili wa Ligi Kuu msimu huu uliamuliwa na mabadiliko hayo, pamoja na ari ya wachezaji wake katika dakika 45 za mwisho.
Amepongeza kiwango cha Simba kipindi cha kwanza, akisema ushindani mkali wa mchezo huo ulitokana na ubora wa wapinzani wao ambao licha ya kupoteza, walionyesha soka safi.
“Tumecheza mchezo mzuri kipindi cha pili, licha ya Simba kucheza vizuri katika kipindi cha kwanza. Ulikuwa mchezo wa ushindani mkubwa kutokana na uwezo wa wapinzani wetu,” alisema Ibenge.
The post MATOLA ASIKITISHWA NA SOWAH, MWALIMU NA MUKWALA appeared first on Soka La Bongo.







