MOROGORO: RAPA Selemani Msindi maarufu Afande Sele amesema ametumiaka miaka 10 ili kumpata mke mwingine bora baada ya kifo cha mke wake wa kwanza.
Afande Sele amefunga ndoa ya kiserikali na Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi Iman Makongoro.
Amesema baada ya kifo cha mke wake wa kwanza na Watoto alikuwa nao aliamua kusubiri kwa miaka 10 akitafakari na kusubiri wakati sahihi hadi akampata Imani na kumuoa.
“Nilisubiri miaka 10 ndiyo nikaingia katika ndoa mimi si mgeni katika ndoa nilishakuwa katika ndoa miaka 10 iliyopita lakini mwezangu alifariki hivyo kwa sasa ninaimani mwanamke niliyemuoa ni wa kufa na kuzikana” alisema Afande Sele.
Aliongeza kwamba ndoa yao ilikuwa ni mjumuiko wa furaha kati ya wasanii na waandishi wa Habari kwa kuwa muoaji yeye ni msanii na mke wake ni mwandishi wa Habari.
“Ilikuwa sherehe fulani hivi nzuri sana nategemea mimi na mke wangu Imani Makongoro tutatimiza misingi na maana halisi ya ndoa kama Mungu anavyopenda iwe kufa na kuzikana,” alisema Afande Sele akiwa na furaha mno.
Wakati Afende Sele anafunga ndoa tayari mtoto wake wa kwanza Tunda ameshamaliza chuo kikuu na sasa anaendelea na shughuli zake za ujenzi wa taifa.
Wasanii mbalimbali wakiwemo wenye majina makubwa katika sanaa ya muziki walihudhuria sherehe za ndoa hiyo iliyofanyika katika Hotel ya Morena akiwemo Stara Thomas, Mr Blue, Dito na Koba waliokuwa wakiunda Kundi la Watu Pori, Majivuni na Kasa Boy waliokuwa wakiunda Kundi la Getho Boys.
Ndoa ya wawili hao ilifungwa Jumamosi Desemba 6, 2025 mbele ya Ofisa Tawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Morogoro Mjini, Hilary Sagara.
The post Afande Sele: Nimetumia miaka 10 kumpata mke bora first appeared on SpotiLEO.






