MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo akisisitiza kuwa timu bado ipo kwenye mwenendo sahihi licha ya kupoteza mchezo mmoja pekee katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika ukurasa kwake wa mtandao wa kijamii, Ahmed amesema hakuna sababu ya wafuasi wa Simba kujihisi wanyonge, kwani kikosi kimeonyesha ubora mkubwa kwenye mechi tano walizocheza mpaka sasa, kikishinda michezo minne na kupoteza mmoja tu.
“Huu ni wastani mzuri, hata kama matarajio ya mashabiki yamekuwa makubwa zaidi msimu huu. sasa wachezaji wako kwenye mapumziko mafupi, mapumziko hayo yanapaswa kuwa ya kimwili pekee huku akili na dhamira za kila mmoja zikiendelea kubaki kazini ili kutathmini namna ya kurejea kwa nguvu mpya na ari ya ushindi,” amesema.
Ahmed aliongeza kuwa mashabiki wa Simba wana matarajio makubwa na wanaitaka timu ifanye vizuri kila mechi, jukumu kubwa liko kwa wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha wanajitoa kikamilifu ili kuyafikia malengo hayo bila kutetereka kutokana na matokeo ya karibuni.
“Klabu itayafanyia kazi maoni, ushauri na hata ukosoaji unaotolewa na wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha utendaji na kuifanya timu iwe imara zaidi ndani na nje ya uwanja. Simba bado ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano yote inashiriki,” amesema.
Ahmed amesema katika Ligi Kuu, Simba imebakiwa na michezo 25, hali inayotoa fursa ya kurekebisha mapungufu na kuongeza ushindani.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, amesema zipo mechi nne muhimu zinazohitaji maandalizi makubwa ili kurejea katika kiwango cha kutisha kilichozoeleka.
Ahmed ameeleza kuwa hakuna sababu ya kukata tamaa au kuona msimu umekuwa mgumu kwa kupoteza mchezo mmoja tu, bado mapema na safari ya mafanikio ya Simba ndiyo kwanza inaendelea kuchanja mbuga.
The post SIMBA HAIJAPOTEZA DIRA YAKE, AHMEDY ALLY appeared first on Soka La Bongo.






