BRUGGE: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amemmiminia sifa nyingi winga wa klabu hiyo Noni Madueke baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Club Brugge nchini Ubelgiji usiku wa kuamkia leo.
Madueke alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali dakika ya 25, likiwa bao la kuvutia ambalo Arteta alilitaja kama bao lililotokana na ubora binafsi. Winga huyo mwenye umri wa miaka 23 aliongeza la pili kipindi cha pili kwa kichwa cha ‘near post’.
Madueke, aliyejiunga na Arsenal akitokea Chelsea mwezi Julai, sasa amefunga mabao matatu katika michezo miwili ya UCL bao lake la kwanza likiwa katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Bayern Munich mwezi uliopita baada ya kurejea kutoka majeraha ya goti.

Alicheza upande wa kulia dhidi ya Brugge, nafasi anayocheza mara nyingi Bukayo Saka, na Arteta amesema ushindani kati yao ni mzuri kwa kiwango cha timu.
Arteta amesema wachezaji hao wanakamilishana kwa ubora wa aina tofauti, akisisitiza kuwa ratiba yao ya mechi kila baada ya siku tatu inahitaji wachezaji walio na nguvu, ubunifu na uthabiti.
“Ni juu ya uimara wa kiwango. Si mechi moja au mbili. Ni unapocheza mechi kumi mfululizo kila baada ya siku tatu na kudumisha kiwango hicho,” amesema.
Vinara hao wa Ligi Kuu England, watawakaribisha Wolverhampton Wanderers katika dimba la Emirates Jumamosi katika mchezo mwepesi wa EPL.
The post “Madueke ni mtu na nusu” – Arteta first appeared on SpotiLEO.







