MADRID: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amewasifu wachezaji wake kwa ustahimilivu na ari ya kupambana baada ya kufanya ‘comeback’ na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku katika dimba la Bernabeu.
Licha ya kuanza mchezo kwa kusuasua na kuonekana kuwa hatarini mbele ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Real Madrid, mabao ya Nico O’Reilly na penalti ya Erling Haaland yaliipatia City pointi tatu, yakifuta bao la mapema la Rodrygo.
Guardiola alikiri kikosi chake kilianza mchezo kwa tempo ya chini katika dakika za mwanzo, lakini akapongeza tabia na uthabiti ulioiwezesha timu kurejea mchezoni na hatimaye kuutawala mchezo kitakwimu.

“Tumecheza hapa mara nyingi, tumecheza vizuri zaidi ya leo na hatukushinda. Katika dakika 25 za kwanza, hadi bao la Nico, walikuwa bora kuliko sisi. Nitachukua matokeo, lakini najua tunapaswa kuwa bora zaidi. Najua Februari na Machi, tukifuzu, kiwango kinachohitajika ni cha juu kuliko hiki.” – Guardiola amesema
Baada ya kuongoza, Manchester City ilionekana kuwa timu yenye utulivu zaidi, huku Jeremy Doku na Phil Foden wakisumbua safu ya ulinzi ya Madrid kipindi cha pili. Guardiola alimpa Doku pongezi maalum.
“Kila tulipopoteza mpira walikuwa hatari, hasa Vinicius Jr. Ilikuwa vizuri kupata bao kwani lilitusaidia kurudi kwenye mchezo. Jeremy Doku alikuwa na kiwango cha juu leo, kama baadhi ya wachezaji wengine pia. Ni ‘experience’ nzuri kwa wachezaji wengi wapya waliocheza hapa kwa mara ya kwanza, uwanja ambao ni mgumu sana.”
“Ninawashukuru sana wachezaji. Nimefurahishwa. Nimekuwa hapa mara nyingi miaka ya hivi karibuni, tumepigana vita vingi, na mara nyingi tumekuwa bora kuliko leo lakini hatukushinda. Huo ndio ukweli.” – ameongeza
City sasa iko nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 13, na Guardiola atatarajia uthabiti huu uendelee katika mechi mbili zilizobaki ili kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.
The post Guardiola akoshwa na kiwango Man City, amtaja Doku first appeared on SpotiLEO.







