RIYADH: MSHAMBULIAJI wa Napoli Rasmus Hojlund alikuwa mhimili muhimu wa ushindi baada ya kuisaidia timu yake kuifunga AC Milan mabao 2-0 katika nusu fainali ya Super Cup ya Italia Alhamisi usiku.
Mchezaji huyo raia wa Denmark alihusika moja kwa moja katika mabao yote mawili, akitengeneza bao la kwanza kipindi cha kwanza kabla ya kufunga mwenyewe baada ya mapumziko na kuzima kabisa matumaini ya mabingwa watetezi wa kombe hilo.
Kwa ushindi huo, Napoli sasa itakutana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Inter Milan na Bologna, itakayochezwa leo Ijumaa, katika fainali itakayopigwa Jumatatu.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa King Saud University ulianza kwa kasi ndogo huku timu zote zikionekana kuwa makini, kila moja ikitafuta namna sahihi ya kuifungua ngome ya mpinzani na mbinu sahihi za mchezo.

Napoli walivunja ukimya dakika ya 39 kupitia David Neres, aliyefunga kwa kumalizia mpira wa Hojlund aliyekimbia upande wa kushoto na kurejesha pasi ya chinichini. Kipa Mike Maignan alijaribu kuokoa lakini aliugusa mpira kwa ncha za vidole na kuuelekeza moja kwa moja kwa mfungaji.
Hojlund aliihakikishia Napoli ushindi dakika ya 64 alipoingia kwa nguvu ndani ya eneo la hatari licha ya presha kutoka kwa beki Koni De Winter, kabla ya kupiga shuti kali kutoka pembe finyu lililomzidi akili Maignan na kutinga wavuni.
Baada ya bao hilo, kasi ya mchezo ilishuka huku timu zote zikisubiri nafasi za kushambulia kwa kushtukiza. Hojlund alitolewa dakika za mwisho na kupokelewa kwa kumbatio kutoka kwa mshambuliaji mwenzake Romelu Lukaku, aliyekuwa benchi baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha tangu Agosti.
Napoli sasa wapo hatua moja tu kuelekea kutwaa taji hilo.
The post Hojlund ashiriki kikamilifu ‘maangamizi’ ya AC Milan first appeared on SpotiLEO.






