UONGOZI wa timu ya Muembe Makumbi City imetuma onyo kali kwa wapinzani wake katika Kundi B la Kombe la Mapinduzi, ikisema haina hofu na timu yoyote ikiwemo Simba SC.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hemed Abdulrahman, kuelekea mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni Zanzibar.
Abdulrahman amesema kuwa Muembe Makumbi imeingia katika kundi gumu lenye Simba SC na Fufuni SC ya Visiwani Zanzibar, lakini hilo halijawavunja moyo wala kupunguza ari ya kikosi chake. Ameeleza kuwa timu yao ipo tayari kwa ushindani mkubwa na inalenga kufanya vyema katika kila mchezo.
Akizungumza kuhusu maandalizi, Abdulrahman amesisitiza kuwa kikosi chao kimejiandaa kikamilifu kwa mashindano hayo. Ameongeza kuwa benchi la ufundi na wachezaji wana imani kubwa kuwa Muembe Makumbi inaweza kuvuka hatua ya makundi na kusonga mbele.
Kwa mujibu wa Abdulrahman, lengo la timu hiyo ni kuanza vyema katika mchezo wa kwanza kwa kupata ushindi dhidi ya Fufuni SC. Ameeleza kuwa ushindi huo utawapa morali ya ziada kuelekea mchezo mgumu dhidi ya Simba SC.
“Tunaenda kuchukua alama tatu katika mechi yetu ya kwanza dhidi ya Fufuni SC, kisha baada ya hapo tunalenga kumfunga Simba. Tunaamini katika kundi letu, timu yetu ndiyo itakayofanya vizuri zaidi,” amesema Abdulrahman
Muembe Makumbi City itaanza kampeni yake ya Kombe la Mapinduzi kwa kuikabili Fufuni SC siku ya Jumatatu, Desemba 29, katika Uwanja wa New Amaan Complex saa 10 jioni. Baada ya hapo, itachuana na Simba SC Januari 3, 2026 saa 2 usiku, katika mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi.
The post TIMU YA MUEMBE MAKUMBI YAIPA ONYO SIMBA appeared first on Soka La Bongo.






