DAR ES SALAAM:MKE wa msanii wa Hip Hop Joseph Haule maarufu kama Professor Jay, anayefahamika kwa jina la Mama Lisa, amempongeza mume wake kwa kutimiza umri wa miaka 50, akieleza upendo wake mkubwa, shukrani na imani yake kwa Mungu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mama Lisa aliandika ujumbe maalumu wa kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Professor Jay, akibainisha kuwa safari ya maisha yao haikuwa rahisi, hasa kutokana na changamoto za kiafya walizopitia katika miaka ya nyuma.
Katika ujumbe huo, alikiri kuwa kulikuwa na nyakati ngumu zilizojaa maumivu na majaribu, lakini alisisitiza kuwa Mungu amekuwa mwaminifu na amemwezesha Professorjay kushinda changamoto hizo na kuendelea kuwa hai, imara na mwenye afya njema.
Ameongeza kuwa sifa na utukufu wote vinamrudia Mwenyezi Mungu kwa rehema na neema zake, huku akiomba aendelee kumbariki mume wake, kumlinda na kumkuza katika safari yake ya maisha binafsi na ya kazi.
Aidha, Mama Lisa ameonesha matumaini makubwa ya kumuona Professor Jay akirejea rasmi katika majukumu yake ya kikazi ifikapo mwaka 2026, akiwa na nguvu mpya na ari ya kuendelea kulitumikia taifa kupitia sanaa na majukumu mengine ya kijamii.
Professor Jay ni mmoja wa wasanii wakongwe na wenye heshima kubwa nchini, ambaye mchango wake katika muziki wa Hip Hop na jamii kwa ujumla umeacha alama isiyofutika.
The post Mama Lisa ampongeza Professor Jay kutimiza miaka 50 first appeared on SpotiLEO.









