BEKI wa Klabu ya Simba, Wilson Nangu, amefunguka na kueleza namna mazoezi na nidhamu aliyoijifunza alipokuwa akiitumikia JKT Tanzania vinavyoendelea kumsaidia katika maisha yake ya soka akiwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Nangu alijiunga na Simba akitokea JKT Tanzania baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu, hatua iliyotokana na msimu mzuri aliouonesha akiwa na timu hiyo ya jeshi, ambapo alifanikiwa kufunga mabao mawili pamoja na kutoa asisti mbili, akionesha uwezo mkubwa katika safu ya ulinzi.
Nangu amesema tofauti kubwa kati ya kucheza JKT Tanzania na Simba ipo kwenye idadi ya mashabiki pamoja na presha ya ushindani, lakini misingi ya kazi, mazoezi na nidhamu aliyoijenga awali imekuwa ikimsaidia kuhimili mazingira hayo mapya.
Ameeleza kuwa mazoezi ya Simba ni ya ushindani mkubwa na yanahitaji umakini wa hali ya juu, lakini kutokana na mafunzo aliyoyapata JKT, ameweza kuendana na kasi ya timu na kujifunza haraka mahitaji ya benchi la ufundi.
Nangu amesisitiza kuwa kupumzika baada ya mazoezi ni jambo muhimu katika kujenga mwili na kurejesha nguvu, huo ni utaratibu aliouzoea tangu akiwa JKT na una mchango mkubwa katika kuimarisha kiwango chake uwanjani.
“Kama unavyojua kazi yetu ni ngumu, mazoezi yanahitaji nguvu nyingi, hivyo kupumzika baada ya mazoezi ni sehemu ya kuhakikisha mwili unarudi katika hali nzuri na kujiandaa kwa changamoto zinazofuata,” amesema Nangu.
Amesema anaendelea kujifunza na kufanya kazi kwa bidii ndani ya Simba, akiamini nidhamu, uvumilivu na mazoezi ya mara kwa mara ndiyo silaha zitakazomsaidia kufikia malengo yake binafsi pamoja na yale ya klabu hiyo kongwe nchini.
The post NANGU AFICHUA KINACHOMBEBA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.




