OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe ametuma ujumbe mzito kwa wapinzani wao Azam FC kuelekea fainali ya Kombe la Mapinduzi, akisisitiza kuwa atakuwepo kwenye mchezo huo muhimu unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka.
Ujumbe huo wa Kamwe umebeba tafsiri pana zaidi, ukimaanisha ujio wa mchezaji mpya wa Yanga, Allan Okello, ambaye ni mali halali wa klabu hiyo akitokea Vipers SC ya Uganda, na tayari yupo kwenye mipango ya kikosi kinachonolewa na Kocha Pedro Goncalves.
Nyota huyo wa kimataifa wa Uganda ametua nchini jana na kuelekea moja kwa moja visiwani Zanzibar, ambako alishuhudia Yanga wakifanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars.
Uwepo wa Okello umeongeza morali ndani ya kikosi cha Wananchi, huku mashabiki wakitarajia kuona mchango wake mkubwa kutokana na uzoefu na ubora alionao katika eneo la kiungo cha ushambuliaji.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu, Okello anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kitakachoshuka dimbani katika mchezo wa fainali dhidi ya Azam FC, endapo taratibu zote zitakamilika kwa wakati.
Fainali hiyo ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuchezwa Januari 13, katika Uwanja wa Gombani Pemba, ambapo Yanga na Azam FC zitachuana kuwania taji hilo huku mvuto wa mchezo ukiongezeka zaidi kutokana na ujio wa Okello.
The post KAMWE ATUMA UJUMBE MZITO AZAM FC appeared first on Soka La Bongo.





