DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva, Saraphina Michaeli ‘Phina’, amesema ukimya wake wa hivi karibuni kwenye shughuli za muziki umetokana na maandalizi ya mambo makubwa aliyokuwa akiyafanya kwa kushirikiana na mpenzi wake, Eni kutoka Nigeria.
Phina ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha picha akiwa pamoja na Eni, akieleza kuwa kipindi walichokuwa kimya kilikuwa na sababu maalumu.
“Tumekuwa kimya kidogo ni kwa sababu tulikuwa tunawaandalia mambo mazuri. Usiku wa AFRIMMA umekuwa wa kipekee sana na umeendelea kutukumbusha kwamba kila kitu kinawezekana,” ameandika Phina.
Msanii huyo amesema tukio la Usiku wa AFRIMMA limekuwa chachu kubwa kwake binafsi na kitaaluma, likimpa motisha ya kuamini ndoto na mipango mikubwa anayoiandaa kwa siku zijazo.
Mashabiki na wadau wa muziki wameendelea kuonesha furaha na kumuunga mkono msanii huyo, wakisubiri kwa hamu kuona ni mambo gani mazuri anayoyapanga kuyatoa kwa ushirikiano na Eni.
Kwa sasa, Phina ameendelea kuwa miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva, huku maisha yake binafsi yakizidi kuvutia macho ya mashabiki wake ndani na nje ya nchi.
The post Phina:Mimi na Eni tulikuwa tunaandaa mambo mazuri first appeared on SpotiLEO.




