LONDON:HATMA ya Axel Disasi na Raheem Sterling ndani ya Chelsea inaweza kubadilika chini ya kocha mpya Liam Rosenior, ambaye ameacha wazi mlango wa kurejea kwao kwenye kikosi cha kwanza.
Rosenior amesema ana heshima kubwa kwa Sterling kutokana na kazi kubwa aliyofanya katika soka, huku akimuelezea Disasi kama mchezaji ambaye amemvutia kwa muda mrefu.
“Raheem ana historia kubwa sana katika soka, namheshimu mno. Axel ni mchezaji ambaye nimempenda kwa muda mrefu. Kwa sasa, lazima niketi nizungumze nao. Pia lazima nizungumze na klabu. Ninasema ukweli kabisa, bado napitia orodha ya vipaumbele vyangu, na nitayafanyia kazi siku chache zijazo,” amesema Rosenior.
Kauli hiyo imekuja wakati ambao kumekuwa na maswali mengi kuhusu nafasi ya wachezaji hao ndani ya mpango mpya wa Chelsea. Badala ya kutoa uamuzi wa haraka, Rosenior ameonesha anataka kwanza mazungumzo ya ana kwa ana kabla ya kuchukua mwelekeo wowote rasmi.
Hii inaacha wazi uwezekano wa Sterling na Disasi kurejea kwenye kikosi cha kwanza, au kufanya maamuzi mapya kulingana na maono ya kocha mpya katika siku chache zijazo.
The post Kuna uwezekano Sterling na Disasi kurejea kikosini first appeared on SpotiLEO.





