KLABU ya Simba SC imefanikiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Senegal, Libasse Gueye, ambaye amejiunga rasmi na Wekundu wa Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi cha Simba kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mashindano ya ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo klabu hiyo inalenga kufanya vizuri zaidi msimu ujao.
Gueye ana uzoefu wa soka la ushindani barani Afrika na anatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Simba SC. Mshambuliaji huyo analeta kasi, nguvu na uwezo wa kufumania nyavu, sifa ambazo zimekuwa zikihitajika ndani ya kikosi hicho.
Simba imemtambulisha rasmi mshambuliaji huyo ni sehemu ya mahitaji ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Steve Barker, ambaye aliwataka viongozi kuboresha kikosi kwa kuongeza wachezaji wenye ubora na uzoefu.
Uongozi wa Simba umeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuijenga timu imara kwa kufanya usajili wa kimkakati, ikiwa ni maandalizi ya kuhakikisha klabu inakuwa na ushindani mkubwa katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Usajili wa Libasse Gueye unaendeleza kaulimbiu ya Simba ya “Nguvu Moja”, ukionesha wazi azma ya klabu hiyo kujenga kikosi chenye ubora, mshikamano na uwezo wa kupigania mafanikio makubwa ndani na nje ya Tanzania.
The post GUEYE SASA NI MNYAMA MSIMBAZI appeared first on Soka La Bongo.





