BEKI wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amesema kikosi cha timu hiyo kimejipanga kuhakikisha kinawapa furaha mashabiki wao katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.
Yanga itakuwa nyumbani Januari 31, 2026, katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa kwenye dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza ugenini.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kikosi hicho, Tshabalala amesema wamejifunza kutokana na makosa yaliyotokea katika mchezo wa kwanza na sasa wanarejea nyumbani wakiwa na lengo la kusawazisha makosa na kupambana kwa nguvu zote.
Amesema licha ya ugumu wa mchezo uliopita, wachezaji walitekeleza maelekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Pedro Goncalves, lakini matokeo hayakuwa yale waliyotarajia.
“Huu ulikuwa mchezo mgumu, tulisimama vizuri katika mipango ya mwalimu, lakini hatukupata matokeo tuliyoyahitaji,” amesema Tshabalala.
Ameongeza kuwa hatua ya makundi ni ndefu na bado kuna nafasi ya kurekebisha hali, huku akiahidi kuwa katika mchezo wa nyumbani watahakikisha wanaibuka na matokeo chanya.
“Hizi ni mechi za makundi, ni marathon. Kuna mchezo mwingine wa marudiano nyumbani dhidi yao, tutahakikisha tunapambana na sisi tunafurahi vizuri,” amesema Tshabalala.
The post TUTAFURAHI MECHI YA NYUMBANI, TSHABALALA appeared first on Soka La Bongo.





