ACCRA, Ghana: Waghana duniani kote wamegeuza kejeli za mitandaoni kuwa sherehe ya kimataifa kwa kulirejesha kwa fahari vazi lao la asili kupitia maadhimisho mapya yanayojulikana kama ‘Fugu Day.’
Kwa mujibu wa BBC, harakati hizo zilichochewa na vita ya kidijitali mtandaoni kati ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kutoka Ghana na Zambia kuhusu vazi la fugu joho la kitamaduni lililosokotwa kwa mikono kutoka Kaskazini mwa Ghana.
Mvutano huo ulianza kwenye majukwaa ya TikTok na X, ambapo baadhi ya wanamitandao na watani mtandaoni walianza kubeza picha za vazi hilo linalovaliwa kwenye harusi na sherehe za kitamaduni.
Vazi hilo la pamba lenye rangi ang’avu na muundo mpana lilifananishwa isivyo haki na nguo za kulalia au mavazi ya filamu za kufikirika, huku baadhi ya maoni yakisema, Kwa nini wanavaa hivyo? Maudhui hayo yalivuna mamilioni ya watazamaji.
Hata hivyo, badala ya kukata tamaa, Waghana waliamua kubadili mkondo wa simulizi hiyo. Kwa umoja wao walitangaza Februari 10 kuwa ‘Fugu Day,’ siku maalum ya kusherehekea na kujivunia urithi wao wa kitamaduni.
Ndani ya saa 48 pekee, lebo za mitandaoni kama #FuguDay na #FuguPride zilianza kutrendi kimataifa, zikikusanya zaidi ya machapisho milioni tano.
Wanadiaspora wa Ghana walijaza mitandao kwa picha za mitindo ya hali ya juu na changamoto za dansi, wakionesha ubunifu wa mavazi hayo kuanzia mitindo ya asili iliyo na mvuto wa kente hadi rangi kali za kisasa na michoro iliyoboreshwa kwa ubunifu wa kisasa.
Mastaa kadhaa maarufu akiwemo Fuse ODG na Efya waliungana na harakati hiyo, wakionesha mavazi yaliyounda daraja kati ya urithi wa kale na mitindo ya sasa.
Mtumiaji mmoja wa X aliandika akifuatisha video ya mwanamitindo aliyevalia fugu akicheza muziki wa Afrobeats:
“Walitudhihaki, sasa wanatuiga.”
Hatimaye, mjadala huo uligeuka kuwa sherehe pana ya urithi wa Kiafrika, huku Wazambia nao wakitumia fursa hiyo kuonesha kwa fahari mavazi yao ya asili yanayojulikana kama Siziba.
Wimbi hilo la kuonesha utamaduni lilivutia hata viongozi wa juu. Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, alionesha nia ya nchi yake kuagiza mavazi ya fugu moja kwa moja kutoka Ghana. Kwa upande wake, Rais wa zamani wa Ghana, John Mahama, alipendekeza Ghana ianze kusafirisha kwa wingi mavazi hayo kwenda Zambia ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Maadhimisho ya Fugu Day yameonesha jinsi jamii zinavyoweza kubadilisha ukosoaji wa mtandaoni kuwa fursa ya kuimarisha utambulisho na kujivunia utamaduni wao, huku yakithibitisha kuwa mitandao ya kijamii inaweza pia kuwa jukwaa la umoja na heshima ya asili za Kiafrika.
The post Waghana Wazindua ‘Fugu Day’ vazi lao la asili, Rais apongeza first appeared on SpotiLEO.




