BAADA ya sintofahamu kuhusu mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Simba SC, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameuingilia kati na kumtaka Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa, kuipa klabu hiyo majibu ya haraka kuhusu kinachoendelea.
Makonda amesema ni muhimu kwa ofisi ya msajili kukamilisha taratibu zote zinazohusu mchakato huo kabla ya mwisho wa mwezi huu, ili kuondoa sintofahamu iliyopo na kuwapa Wanasimba uhakika wa mustakabali wa timu yao.
“Msajili wa michezo nilitaka mkamilishe taratibu za Simba. Na nilitaka niwahakikishie kwamba katika kipindi ambacho sheria na kanuni zitafuatwa sana ni hiki cha uongozi wangu,” amesema Makonda, akisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya kisheria katika maamuzi yote.
Aidha, Waziri huyo ameongeza kuwa matarajio yake ni kuona majibu hayo yakitolewa kwa wakati, ili kuondoa wasiwasi miongoni mwa mashabiki na wadau wa klabu hiyo.
“Kamilisha na ikiwezekana kabla ya mwezi huu uwape majibu Wanasimba. Tunachotaka sisi ni kuona timu hizi zikifanya vizuri. Kabla ya mwezi huu, jambo hili liwe limekamilika,” amesisitiza.
Kauli hiyo ya Waziri inakuja katika kipindi ambacho Simba SC ipo kwenye hatua ya maboresho ya mfumo wa uendeshaji, huku mashabiki wengi wakihitaji uwazi na uwajibikaji katika mchakato huo muhimu kwa mustakabali wa klabu yao.
The post PRESHA KWA MSAJILI, WAZIRI ATAKA HATMA YA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.



