UONGOZI wa klabu ya Simba umefanikiwa kumuongezea mkataba beki wake tegemeo Rushine De Reuck baada ya kukamilisha taratibu zote za kipengele cha kuongeza muda kilichokuwapo kwenye makubaliano ya awali.
Hatua hiyo inaashiria kuendelea kwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili huku uongozi wa timu ukionyesha imani kubwa kwa mchezaji huyo raia wa Afrika Kusini.
Awali Rushine alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya kikosi cha Simba uliokuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mwingine endapo pande zote zingekubaliana. Baada ya tathmini ya mwenendo wake uwanjani na mchango wake katika safu ya ulinzi, uongozi wa klabu umeamua kuamsha kipengele hicho na kumfanya aendelee kuitumikia timu hiyo.
Imeelezwa kuwa beki huyo amekuwa mmoja wa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Simba tangu alipojiunga na klabu hiyo. Uwezo wake wa kusoma mchezo, kupiga mipira ya juu pamoja na uzoefu wake mkubwa umeifanya Simba kuwa na uimara zaidi katika safu ya nyuma.
Mtoa habari huyo amesema hatua ya kumuongezea mkataba inatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuimarisha kikosi chake kwa muda mrefu. Simba imekuwa ikifanya maboresho katika kikosi chake ili kuhakikisha inabaki kuwa na ushindani mkubwa katika mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa.
“Rushein amekuwa akionyesha kujitoa kwa kiwango kikubwa kila anapopewa nafasi ya kucheza. Nidhamu yake ndani na nje ya uwanja imekuwa mfano kwa wachezaji wengine na moja ya sababu zilizochangia kupewa nafasi ya kuendelea kusalia klabuni hapo,” amesema mtoa habari.
Ameongeza kuwa sasa kila kitu kimekamilika rasmi na beki huyo ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwa msimu ujao. Hatua hiyo inaipa timu hiyo utulivu katika safu ya ulinzi huku ikijiandaa na malengo makubwa ya ushindani katika ligi na mashindano mengine.
The post RUSHINE MKATABA MWINGINE SIMBA, ULINZI WAIMARIKA appeared first on SOKALEO.



