Na. Mwandishi wetu: Shinyanga
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama ili kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo.
“Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya Lugha ya Alama kwa kuchukua hatua za muda mfupi, kati na mrefu. Hatua za muda mfupi ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watoa huduma katika Sekta mbalimbali. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetoa mafunzo kwa watoa huduma za Afya, Maafisia Ustawi wa Jamii, Walimu wa Shule ya Msingi na sekondari“ amesema.
Mhe. Katambi amebainisha hayo Septemba 28, 2024 katika Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika kwenye Uwanja wa Kambarage Manispaa ya Shinyanga, ambayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo “TUMIA LUGHA YA ALAMA KUTIMIZA HAKI YA LUGHA YA ALAMA.”
Aidha, amelitaka Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ikamilishe mwongozo wa Wakalimani wa Lugha ya Alama ambao utachangia kukua na kuenea kwa lugha ya alama pamoja na tasnia ya ukalimani.
Vile vile, ametoa rai kwa vyombo vya habari vya kitaifa vinapotangaza matukio ya kitaifa na taarifa za habari kuhakikisha Wanakuwa na Wakalimani wa lugha ya alama, Wizara na Taasisi kuchukue hatua ya kuwapeleka Watumishi kwenda kupata mafunzo ya muda mfupi ya Lugha ya Alama.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Selina Mlemba ameipongeza serikali kwa kuendelea kutambua umuhimu wa lugha ya alama na hivyo kutenga siku maalumu kwa ajili ya siku hiyo Pamoja na kutenga fungu kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu.
Naye, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa (UNDP) Ghati Horombe, amesema Shirika hilo linathamini na kutambua juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu na serikali kwa ujumla katika kuhakikisha ujumuishwaji kijamii, kisiasa, kiuchumi na upatikanaji wa haki, kwa Watu wenye Ulemavu.