Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imefanya mazungumzo na mwendeshaji wa Kitalu cha Mnazi Bay (Kampuni ya Maurel et Prom Exploration Production Tanzania Ltd) kujadili mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotarajiwa kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 2025.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Septemba 30, 2024 katika Ofisi za PURA Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa PURA.
Miongoni mwa wajumbe walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Bw. Simon Nkenyeli ambaye ni Meneja wa Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia kutoka PURA na Meneja Mkuu wa M&P Bw. Sylvain Pichelin.
Katika kikao hicho, M&P ilitoa ufafanuzi wa bajeti ya mradi, hatua muhimu kabla ya PURA kutoa idhini ya matumizi ya fedha kwa ajili ya mradi huo. Mradi unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani Milioni 80.2
Kati ya visima vitakavyochimbwa, visima viwili (MB5 na MS2) vitakuwa visima vya uzalishaji (infill) wakati kisima kimoja (Kasa) kitakuwa kisima cha utafutaji.
Kuelekea utekelezaji wa mradi, tathmini ya athari kwa mazingira imekamilika na zoezi la fidia kwa wananchi watakaopisha mradi linatarajiwa kuanza mapema mara baada ya uhakiki kukamilika.
PURA na M&P zilijadilia pia ushiriki wa watanzania na watoa huduma wa kitanzania katika zabuni zinazotokana na mradi huo.
Katika eneo hili, PURA iliitaka M&P kuhakikisha inazingatia matakwa ya Sheria kuhusu ushiriki wa watanzania. Aidha, PURA ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha watanzania na watoa huduma wa kitanzania wanashiriki kikamilifu.
Kitalu cha Mnazi Bay kina visima vitano vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 74.24 kwa siku (kwa mwezi Septemba)
Wabia katika Kitalu hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni M&P (ambaye ni mwendeshaji) mwenye ushiriki wa asilimia 60 katika shughuli za uzalishaji na TPDC mwenye asilimia 40.
Uchorongaji wa visima vitatu vipya utawezesha kuimarisha uzalishaji (maintenance of production plateau) na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia kuhusu mashapo yaliyo katika Kitalu hicho.