Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Ester Mahame, ametembelea kambi ya matibabu inayotolewa na Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika hospitali ya wilaya ya Vwawa kwa lengo la kujionea hali ya utoaji huduma pamoja na kuonge na kuwafariji wagonjwa waliojitokeza kupatiwa matibabu katika kambi hiyo, ambayo itakaa mkoani Songwe kwa siku 7.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mahame amesisitiza umuhimu wa maboresho wakubwa ya huduma za afya nchini yakiyofanyika na kumpongeza Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani na Serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira mazuri ambayo yanawawezesha vijana wengi kufikia viwango vya udaktari bingwa katika magonjwa mbalimbali.
“Nina kila sababu ya kuipongeza serikali kwa jitihada zake za kuimarisha elimu na mafunzo kwa vijana wetu, ambapo sasa tunashuhudia madaktari bingwa wa umri mdogo wakiwapatia wananchi huduma stahiki,” alisema. Mhe. Mahame
Aidha, ametoa wito kwa madaktari hao na wahudumu wa afya kuwa na moyo wa kujitolea katika kutimiza wajibu wao wa kuokoa maisha ya watu.
“Mnafanya kazi ya kuokoa uhai wa watu kupitia uwezo wa Mungu mwenyewe, kwahiyo tunawaombea sana ili muweze kufanikisha malengo yenu,” aliongeza.
Mhe. Mahame amesifu upendo wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Tanzania, akisema kuwa Serikali yake inaonyesha kujali na kuhudumia watu kwa moyo wote.
“Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha upendo mkubwa kwa wananchi kupitia miradi kama hii, ambayo inalenga kuboresha afya na ustawi wa jamii yetu,” alisema.
Vilevile, Mhe. Ester ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Wizara ya Afya kwa uratibu mzuri wa kambi hii ya matibabu, ambayo inaonesha juhudi zao za kuwafikia wananchi popote walipo.
“Ninawashukuru sana Wizara ya Afya kwa kazi yenu nzuri na uzito mlio nao katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila vikwazo,” alihitimisha.
Mhe. Mahame amewatakia kila la kheri madaktari hao na kuwashauri kuendelea kuboresha huduma zao kwa wananchi wa Wilaya ya Mbozi.
Amesema kwamba ni matarajio yake kuwa mwisho wa kambi hiyo, kutakuwa na matokeo mazuri yatakayosababisha furaha kwa wananchi ambao watafaidika na huduma zinazotolewa katika kambi hiyo.