Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, ameendelea na ziara yake ya kikazi ambapo amekutana na wafanyakazi wa NHC Mkoa wa Mtwara.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Bw. Abdallah amewataka kuongeza juhudi katika kazi zao ili kuliwezesha Shirika kuleta tija zaidi na kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi. Pia, amesisitiza umuhimu wa NHC kuendelea kulipa gawio kubwa kwa serikali, ambalo linategemea utendaji bora wa wafanyakazi katika kila mkoa.
Ziara ya Mkurugenzi Mkuu inalenga kukagua miradi ya Shirika pamoja na utendaji kazi wa ofisi za NHC mikoani, na leo anamalizia ziara yake mkoani Lindi.
Katika hotuba yake, Bw. Abdallah amepongeza wafanyakazi wa NHC Mtwara kwa kazi nzuri wanayofanya katika matengenezo ya nyumba na kwa ubunifu wao ambao umechangia kuongeza mapato ya mkoa huo.
Wafanyakazi wa NHC Mtwara walimshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kuonyesha kujali maslahi yao na kwa kutoa motisha katika kazi.
Waliahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kuongeza tija kwa Shirika na kuchangia maendeleo ya NHC kwa ujumla.
Ziara hii imekuwa fursa kwa Mkurugenzi Mkuu kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wafanyakazi, kujua changamoto zao, na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika katika miradi yake mbalimbali.
Wafanyakazi wa shirika la nyumba NHC Mkoani Mtwara wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa shirika Hilo Bw. Hamad Abdallah.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua nyumba za makazi na ofisi zinazomilikiwa na NHC katika eneo la Rahaleo katika Manispaa ya Mtwara. Katika ukaguzi huo ni Meneja wa NHC Mtwara Bw. Joseph John Mwabukuzi