Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 2, 2024 jijini Dar es Salaam.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kupitia Dalali wa Mahakama wanatarajiwa kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba pamoja na kuwafungulia kesi ya madai mahakamani ili kuhakikisha wanalipwa shilingi bilioni 14.8 ambazo ni malimbukizi ya madeni kutoka kwa wapangaji wote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 2, 2024 jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa zoezi la kuwaondoa wadai sugu katika nyumba linatarajiwa kuanza Oktoba 7, 2024 katika Mkoa wa Dodoma, Mwanza, Arusha pamoja na Mara.
Arch. Kondoro amesema kuwa tayari dalali wa mahakama amefata taratibu zote za kuwaondoa wadaiwa sugu 648 katika mikoa hiyo, huku akieleza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku 14 kuanzia siku ambayo wadaiwa wamepewa taarifa ya kuondoka.
“Zoezi hili litafanyika nchi nzima kuanzia siku ambayo taarifa ilitolewa Septemba 17, 2024, TBA itaendelea kuwachukua hatua za kisheria dhidi ya wapangaji wote wanaodaiwa ikiwemo kuwaondoa kwenye nyumba wadaiwa sugu kupitia dalali wa mahakama” amesema Arch. Kondoro.
Arch. Kandoro amesema kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya wateja kutolipa kodi ya pango kwa wakati na kusababisha kuwa malimbukizi makubwa ya madeni na kuikosesha mapato TBA.
Amesema kuwa malimbukizi ya madeni yamekuwa kikwanza kwa utekeleza wa TBA katika maeneo mbalimbali ikiwemo kufanya ukarabati nyumba pamoja na kujenga nyumba mpya.
“Tunaendelea na juhudi mbalimbali za ikiwemo kuwakata mishahara watumishi wa umma ambao wamepanga nyumba za TBA kulingana na makubaliano ya mkataba ili waweze kuepuka malimbukizi ya kodi” Arch. Kandoro.
Ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi TBA wameanzisha mfumo mpya wa kieletroniki wa usimamizi wa miliki za serikali tolelo la pili ambalo linafanyiwa majaribio jiji la Dar es Salaam, ambapo faida ya mfumo huu unatoa riba ya kwa miezi mitatu kwa mpangaji kukaa bila kulipa pango.