Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa majadilino ya mashirikiano kati ya Tanzania na Japan. Mkutano huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 03, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JINCC).
SERIKALI ya Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na Japan hususan katika Sekta ya miundombinu ambapo Tanzania inaendelea na mazungumzo na nchi hiyoili kushirikiana katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano wa magari katika miji na majiji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo Oktoba 03, 2024 wakati akifungua mkutano wa mashirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Japan wakijadili namna ya kushirikiana na Kampuni za hapa nchini kwaajili ya kupanga kimkakati katika ujenzi wa miundombinu ubora.
Amesema Tanzania imeanza mazungumzo na Japan ya kushirikiana katika usanifu na ujenzi wa barabara ya juu (FlyOver) katika eneo la makutano ya barabara la Moroco jijini Dar es Salaam itakayopunguza msongamano wa magari na kurahisisha shughuli za kiuchumi nchini.
“Sasa hivi tunaendelea na mazungumzo na Japan kuhusu ujenzi wa Flyover ya Moroco kwa kufanya usanifu na ujenzi pamoja na kuboresha maeneo mengine yenye mapishano ya barabara ili kupunguza matumizi ya taa za barabarani ambazo sio suluhisho la muda mrefu.” Amesema Bashungwa
Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua nchi kwa kuweka mazingira wezeshi na kuvutia uwekezaji na biashara kwa nchi zingine kwa kuimarisha ushirikiano na upatikanaji wa masoko kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Umoja wa Soko la Afrika.
Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji mbalimbali wanaofika nchini kuwekeza, kufanya biashara na kuondoa urasimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameeleza kuwa maendeleo ya nchi yoyote yanategemea sana sekta ya usafiri kwani ni kiungo muhimu kwa biashara ya ndani na ya kimataifa ambapo kwa sasa Tanzania ina jukumu muhimu kama lango la kimataifa kwa baadhi ya nchi jirani ili kurahisisha usafirishaji na upatikanaji wa soko la kimataifa.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda ameeleza umuhimu wa mkutano huo ambao umewakutanisha wabobezi katika ujenzi wa miundombinu bora na ya kudumu inayoweza kuhimili majanga kama vile matetemeko ya ardhi na vimbunga kutoka nchi ya Japan na hivyo watasaidia kutoa michango na uzoefu kwa makampuni ya ujenzi kwa nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania katika ujenzi wa miundombinu yote nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC)Gilead Teri akizungumza katika Mkutano huo amesema kuwa Wawekezaji 60 wamekuja kuitika wito wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pia baada ya TIC kufanya ziara ya kuhamasisha uwekezaji nchini Japan.
Amesema walikutana naJumuiya ya Wakandarasi pamoja na jumuiya ya kampuni zinazohusiana na uuzaji wa bidhaa za ujenzi Japan kuja nchini Tanzania.
“Leo tumekaribisha Kampuni zaidi ya 100 za kitanzania kuja kukutana na ujio wa kampuni 60 kutoka Japan wakiwa na malengo ya kubadilishana uzoefu wa namna gani Kampuni za Japan zimeweza kuongeza ubora wa miradi yao pamoja na ujenzi wa miundombinu hasa kwenye mazingira magumu.”
Pia ni Kushirikiana na kuunda umoja wa Kampuni za Japan pamoja na Tanzania ili waweze kufanya kazi pamoja hapa nchini kwa maendeleo ya Wajapan na watanzania.
Wakati huo huo Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda na Balozi wa Japan nchini Tanzania Misawa Yasushi wamezindua hati maalumu ya ardhi ya Uwekezaji kwa Wajapan iliyopo katika kiwanda cha Kamal kilichopo Kerege Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda(wa pili kushoto na Balozi wa Japan nchini Tanzania Misawa Yasushi (kulia ) wakizindua hati maalumu ya ardhi ya Uwekezaji kwa Wajapan iliyopo katika kiwanda cha Kamal kilichopo Kerege Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani wakati wa Mkutano uliowakutanisha ujumbe wa wanachama 60 kutoka nchini Japan wawekezaji wa Tanzania kujadili fursa zilizopo na kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 03, 2024 wakati wa Mkutano uliowakutanisha ujumbe wa wanachama 60 kutoka nchini Japan na wawekezaji wa Tanzania kujadili fursa zilizopo na kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Baadhi ya Matukio mbalimbali katika Mkutano uliowakutanisha ujumbe wa wanachama 60 kutoka nchini Japan na wawekezaji wa Tanzania kujadili fursa zilizopo na kuwekeza katika sekta mbalimbali.