Wananchi wa vijiji vya Msolwa Kalengakelo na kitongoji cha Mkuyuni katika kijiji cha Chisano halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro wamevamia maeneo yaliyotengwa na serikali kwa matumizi ya ufugaji pamoja na malisho ya mifugo wakilalamikia serikali za vijiji hivyo kupitisha mpango wa matumizi Bora ya ardhi bila kuwashirikisha.
Wakiongea mbele ya Kamishna wa ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Idrisa Kayera aliyefika katika kijiji cha Kalengakelo kufuatia agizo la waziri wa ardhi kumtaka afike kusikiliza malalamiko ya wananchi hao ambao wameeleza kuwa maeneo Yao ya kilimo yamechukuliwa kufuatia mpango wa matumizi Bora ya ardhi uliopitishwa mwaka 2014.
Kwa mujibu wa madai Yao mpango huo haukuwashirikisha, malalamiko ambayo yalikanushwa na baadhi ya watendaji wa vijiji kulingana na vitabu vilivyochapishwa Wakati wa uandaaji wa mpango huo uliofadhiliwa na Wizara ya Ardhi kupitia mradi wa LTSP.
Akitaka kujua uhalali wa umiliki wa maeneo ya wananchi hao Kamishna wa ardhi aliwataka wananchi Wenye vielelezo vya umiliki waviwasilishe kwake. Wananchi hao waliwasilisha stakabadhi za kununua maeneo Hayo ambapo alibaini kuna mapungufu kwenye vielelezo vilivyowasilishwa kwa kuwa hakuna mihutasari ya Halmashauri na mkutano mkuu wa vijiji iliyodhinisha kuwapatia maeneo hayo. wanabchi akiwemo aliyekuwa mtendaji wa kijiji cha Msorwa Emmanuel Holo aliyejiidhinishia umiliki wa heka 32.
Hollo aliyekuwa mtendaji wa kijiji cha Msolwa ambaye pia alipitisha mpango wa matumizi ya ardhi wa Kijiji hicho mwaka 2014 amebainika kughushi baadhi ya nyaraka ikiwemo risiti za malipo ya maeneo na kujiandikia barua ya kupata ekari hizo, bila kuzingatia mgongano wa maslahi (conflict of Interest).
Ekari hizo 32 anazodai Holo zipo ndani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho na viongozi wa kijiji wanashaka hata kama fedha anazodaiwa kulipa ziliingia katika akaunti za kijiji kipindi akiwa madarakani.
Aidha kwa mujibu wa Abumel Kabelege Mwenyekiti wa Kijiji cha Msolwa alieleza kuwa, “Kipindi Holo akiwa mtendaji wa kijiji cha Msolwa mkutano mkuu uliamua kumpa shamba la ekari 6 tuu ambapo baadae alijiidhinishia ekari zingine 32 ndani ya eneo la malisho bila ridhaa ya mkutano mkuu.
Deodatus Mngungusi ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Samora ameeleza kuwa migogoro hiyo asilimia kubwa inachochewa na wamiliki Wenye maeneo makubwa wanayoyamiliki kinyume cha Sheria ambao wanatoka nje ya vijiji vyao , ambao wanaowashawishi wanavijiji kuvamia maeneo yaliyotengwa na kusababisha migogoro baina ya serikali za vijiji na wananchi.
“Kuna watu Wana eka zaidi ya 100 na hawajafuata utaratibu wa kumiliki Hayo maeneo hawa ndio wanaotuletea hii migogoro na ndio wanaowashawishi hawa wazee na ndio wanaotengeneza hii migogoro na wanatoka nje ya vijiji vyetu,”.
Kamishna wa ardhi akawataka wananchi hao kueleza ukweli ambapo alieleza kuwa migogoro hii hua inakosa usuluhishi wa haraka kutokana na wananchi wengi kuongea uongo pale wanapowasilisha malalamiko Yao huku wakikosa vielelezo muhimu vya umiliki wa ardhi ambapo aliwapa elimu ya taratibu za kufuata wanapohitaji kumiliki ardhi ikiwemo,kuwasilisha maombi Yao katika ofisi za kijiji husika,kujadiliwa na mkutano Mkuu wa kijiji na baadae kupatiwa muhtasari unaohalalisha umiliki wa ardhi.
Aidha Kamishna Msaidizi huyo alimuagiza katibu Tarafa aliyeudhiria kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, kufikisha suala Hili kwa vyombo vya uchunguzi ili hatua zichukuliwe dhidi ya wanaochafua Serikali kwa kuanzisha migogoro ya kubumba ndani ya jamii kwa kughushi nyaraka na kutozingatia mipango ya matumizi Bora ya Ardhi waliyokubaliana.
“Sasa natoa maelekezo kwa vyombo husika kupitia kwa katibu Tarafa kuhakikisha wanawachunguza wote walioghushi nyaraka za umiliki wa ardhi kwasababu hawa ndio wanaochochea migogoro inayoichafua serikali,tunapokuja kusikiliza malalamiko ya wananchi kikubwa tunachotaka ni ukweli, ongea ukweli leta vielelezo vyako vinavyoonesha umiliki halali wa ardhi yako Alafu sisi tuone wapi unaonewa tutatue tatizo lako” alisema.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo Kamishna wa ardhi alifika katika mashamba yaliyo vamiwa kuona Hali halisi ambapo alibaini mengine mapya ikiwemo kushirikishwa kwa watendaji wa vijiji kuuza maeneo kiholela bila kufuata taratibu.
Aidha Kamishna akaendelea kuwakumbusha wenyeviti na watendaji wa vijiji,vitongoji na hata wajumbe wa serikali za vijiji kuwa ni marufuku kujichikulia maamuzi ya kuuza maeneo bila kupitishwa na mkutano mkuu wa vijiji kwani ndio imekua chanzo kikubwa cha migogoro mara kwa mara.
“Nimesikiliza haya yote nimegundua shida iko kwa viongozi wa vijiji ambao mmeifanya ardhi kuwa kama miliki yenu,kitu ambacho sio Sawa,sasa niwakumbishe tuu kuwa ardhi sio Mali ya mtu mmoja unapotaka kuuza ardhi ni lazima mfuate utaratibu uliowekwa na serikali ili kuepusha hii migogoro”
Kamishna akawataka wananchi kufuata Sheria za umiliki wa ardhi kwakua serikali haitatambua umiliki wa eneo ambalo halitakua na vielelezo vinavyotakiwa pale unaponunua ardhi.