Na Farida Mangube
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amewataka Wataalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuimarisha juhudi za utunzaji na uendelezaji wa misitu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho ya miaka 50 ya Kitivo cha Mafunzo ya Misitu cha SUA, Mhe. Malima alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa misitu ili kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinanufaika na rasilimali za misitu na mazingira kwa ujumla. Alieleza kuwa uharibifu wa misitu, unaosababishwa na shughuli za binadamu kama uchomaji mkaa, ukataji kuni, na kilimo maeneo ya pembezoni mwa miji, unahatarisha mazingira na ustawi wa jamii.
Mhe. Malima alitoa wito kwa Wataalamu wa SUA kuelimisha jamii kuhusu athari za uharibifu wa misitu na kuhimiza utekelezaji wa sheria za kulinda rasilimali hizi.
Kwa upande wake, Bi. Metrida Kaijage, Mtaalamu wa Sheria za Misitu kutoka SUA, alisisitiza wajibu wa wataalamu wa misitu katika kutunga miswada na kuishauri serikali ili kuhakikisha matumizi sahihi ya misitu. Alizitaka pia taasisi kama SUA kutafuta ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuimarisha uratibu wa uhifadhi wa misitu.
“Natumaini wataalamu wa SUA wataendelea kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto za kimazingira na kisayansi zinazoathiri misitu na mazao yake,” alisema Bi. Kaijage.
Prof. August Temu, Mtaalamu wa Misitu kutoka SUA, alibainisha kuwa Tanzania inafanya maendeleo mazuri katika utunzaji wa misitu. Alisema SUA inaendelea kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia.