Wasanii wamesisitizwa kuandaa kazi zenye kuzingatia maadili, uadirifu, uzalendo, uelimishaji na ukosoaji kwa jamii katika kazi zao za sanaa wanazozifanya
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa kikao chake na wasanii wa wilaya ya Ilemela kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za CCM kata ya Buswelu ambapo amefafanua kuwa kazi kubwa ya wasanii ni kuielimisha jamii dhidi ya mambo yasiyofaa tofauti na wasanii wengi wa nyakati hizi ambao wamekuwa wakiandaa kazi zisizoishi muda mrefu na kuwa na manufaa kwa jamii
‘.. Sanaa mnayoifanya ina mafunzo gani katika jamii, Zipo nyimbo za kina Baraka Mwinshehe na wengine zilikuwa zinatoa mafunzo ambayo mtu akisikiliza anayapata, Unaweza ukawa mchekeshaji lakini katika kuchekesha kuwe na ujumbe wenye maadili, unaweza kuwa mtunzi wa nyimbo lakini nyimbo unazoimba ziisaidie jamii ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amewaasa wasanii hao kuwa wamoja, kutambulika kisheria na kutumia fursa zilizopo za mikopo ya halmashauri kwaajili ya kujikwamua kiuchumi sanjari na kujitokeza katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kujiandikisha katika daftari la mkazi kwaajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024
Mwashum Ismail ni mwenyekiti wa chama cha wasanii wilaya ya Ilemela ambapo amemshukuru mbunge huyo kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii hao pamoja na namna anavyoshiriki katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili
Nae diwani wa viti maalum kata ya Buswelu Bi Winfrida Gyunda mbali na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazozifanya katika jamii amewataka wasanii hao kuacha kulalamika na badala yake kushirikiana na serikali katika kujiletea maendeleo binafsi na jamii kwa ujumla
Mbunge wa Jimbo la Ilemela amewachangia wasanii hao kiasi cha fedha kwaajili ya mashindano wanayotarajia kushiriki hivi karibuni, chakula na kompyuta mpakato kwaajili ya shughuli zao za kila siku