Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Nombo ndio Mgeni Rasmi
Mkurugenzi wa Costech, Dr. Amos Nungu.
…………….
Serikali ya Tanzania imeendelea kuongeza uwekezaji mwaka hadi mwaka ili kuimarisha mchango wa sayansi, teknolojia, na ubunifu katika kustawisha uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya Watanzania.
Akizungumza leo, Oktoba 4, 2024, wakati wa uzinduzi wa miongozo minne ya utafiti na ubunifu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Bi. Carolyne Nombo, aliipongeza Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) kwa kuandaa miongozo hiyo. Bi. Nombo alieleza kuwa tafiti na ubunifu ni nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Tafiti na ubunifu ni nyenzo muhimu sana katika kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Nchi zilizoendelea duniani zimepiga hatua kubwa kutokana na uratibu na uwekezaji madhubuti katika masuala ya sayansi, teknolojia, na ubunifu,” alisema Bi. Nombo.
Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Bi. Nombo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu, sayansi, na teknolojia. Alisisitiza dhamira ya serikali kuongeza wawekezaji katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Naye Mkurugenzi wa Costech, Dr. Amos Nungu, alisema tume yake itatekeleza kwa umakini maelekezo ya serikali, akibainisha kuwa miongozo minne iliyozinduliwa itasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha tija inayokusudiwa inafikiwa.
“Miongozo hii imezinduliwa wakati muafaka, na tutahakikisha inasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu ili kufikia malengo ya taifa,” alisema Dr. Nungu.
Miongozo minne iliyozinduliwa ni Muongozo wa Kitaifa wa Kushirikiana kati ya Taasisi za Elimu ya Juu, Tafiti na Viwanda; Muongozo wa Kitaifa wa Upatikanaji, Hifadhi, na Usambazaji wa Takwimu za Sayansi na Teknolojia; Muongozo wa Taifa wa Uwezo wa Utafiti wa Kisayansi; na Muongozo wa Taifa wa Ubunifu.