Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa viongozi wa dini wanaoeleza waumini wao kuhusu maendeleo kwa kuhimiza umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2024 katika Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre wa Dkt. Faustine Kamugisha iliyofanyika Kijiji cha Kyamulaile, Wilaya Bukoba Mkoani Kagera.
“Serikali yetu inathamini sana mchango wa viongozi wa dini wanaoelekeza watu kwenye maendeleo ili tujenge nchi ya watu wanaopendana na kuthaminiana,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Kuwa na dini tofauti kwetu si tatizo, umoja wetu tuutunze tuendelee kukumbushana kuwa hatuna taifa lingine na mwaka huu tutakua na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tunadi sera zetu kwa ustaarabu.”
Dkt. Biteko ametoa wito kwa waumini wa Parokia ya Minziro kuendelea kushirikiana na kumsaidia Padre Kamugisha ili afanye kazi yake ya utume vizuri “ Wakatoliki wote na sisi sauti zetu zikawe za kumfariji Padre huyu, ziwe sauti chanya kwenye utume wake.”
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa anamtakia Padre huyo kila la heri na anampongeza kwa kazi kubwa anayofanya katika kanisa na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini ikiwemo Kanisa Katoliki huku akishukuru mchango wa kanisa hilo katika huduma za jamii.
“ Tunatambua na kuthamini mchango wenu katika elimu kwa kutoa elimu bora na shule za kanisa hili zimekuwa zikifanya vizuri na kwa upande wa hospitali mfano Hospitali ya Kagondo imekuwa ikitoa huduma bora kwa wananchi, imetupa chachu na sisi kuboresha hospitali yetu,” amesema Mhe. Mwassa
Askofu Mkuu wa Jimbo la Bukoba, Jovitus Mwijage amempongeza Padre Faustine Kamugisha kwa kutimiza miaka 25 ya upadre na kusema kuwa Padre huyo amekuwa na juhudi katika kufanya utume wake na kujiendeleza katika masuala mbalimbali.
“ Tunakushukuru na kumshukuru Mungu kwa zawadi aliyokupatia, utume huu usiishie hapa uendelee na sisi tutakukumbuka katika sala ili hudumu katika utume huu”, amesema Askofu Mwijage.
Pia, Askofu Mwijage amesema kuwa Tanzania ni nchi isiyo na dini ila watu wake wana dini hivyo amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa kuhudhuria katika misa hiyo jambo linaloashiria umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akitoa shukrani zake, Padre, Dkt. Faustine Kamugisha amemshukuru Mungu kwa kumsaidia kufikia hatua hiyo ya kutimiza miaka 25 ya upadre.
Aidha, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Kanisa na Serikali hata alipoomba umeme na maji katika vituo vya hija Serikali iliweza kusaidia kufikisha huduma hizo.
Sambamba na kuwashukuru Maaskofu mbalimbali waliomsaidia katika kufikia hatua ya miaka 25 ya upadre, amemshukuru pia Dkt. Biteko kwa kuhudhuria misa hiyo.
Padre wa Jimbo la Tanga, Jonathan Mutalemwa wakati akihubiri katika misa hiyo amesema kuwa kufikia siku hiyo ni ahadi ya Mungu na kuwa tukio hilo ni muhimu kwa kuwa ni kitu ambacho baba yake mzazi Padre Kamugisha alikitamani maishani mwake.
“Tunapofanya jubilei hii leo tujue famili ni kanisa dogo, huyu tunamsheherekea leo ni Timotheo kwa kuwa imani aliyonayo na ujasiri ulianzia kwa mzazi wake ambaye alifanya shughuli nyingi za kusaidia Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba ,” amesema Padre Mutalemwa.
Ameongeza kuwa sherehe hiyo ni ishara ya kuwa Padre Kamugisha ameacha alama katika utume wake wa kazi ya ukuhani katika kipindi chote cha miaka 25.
Sambamba na misa hiyo ya Jubilei ya Miaka 25 ya Padre Kamugisha, Dkt. Biteko amezindua kitabu kinachoitwa “ Hatupangi Kushindwa, Tunashindwa Kupanga” kilichoandikwa na Padre huyo.