Na Gustaph Swai -Songea
Meneja wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Tawi la Songea Dkt. Bakari Mashaka amebainisha kuwa chuo hicho kinaleta mradi Mkubwa wa bilioni 18.5 za Kitanzania ambazo ni fedha za Serikali kujenga Chuo Kikuu Katika Mtaa wa Pambazuko kata ya Tanga Manispaa ya Songea.
Ameeleza hayo katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya Michezo ambapo Chuo Kikuu hicho kimetoa mipira ya Miguu saba kwa timu za mpira wa Miguu zilizopo katika mtaa wa Pambazuko Kata ya Tanga, Manispaa ya Songea.
“Tunaleta mradi Mkubwa wa takribani shilingi bilioni 18.5 za Kitanzania, ni fedha za Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu ambaye ameweka lengo Kila Mkoa uwe na Chuo Kikuu”, alisema.
Amebainisha kuwa Chuo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi kwa kuanzia 5,000 mpaka 10,000.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa mradi huo utaanza kutekelezwa mapema kuanzia sasa mara baada ya taratibu za zabuni kukamilika na unatarajiwa kumalizika baada ya miezi 18.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pambazuko, Nickson Mhagama ameeleza kuwa wananchi wa Kijiji hiko wameupokea Mradi huo kwa furaha kubwa na wataendelea kushirikiana na Chuo katika utekelezaji wa mradi huo.
Ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu hicho kwa kuwaelimisha Wananchi juu ya faida za mradi huo.
Chuo Cha Uhasibu Arusha kina eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 26.5 katika Mtaa wa Pambazuko kata ya Tanga Manispaa ya Songea ambapo ndipo mradi wa Tawi la Songea utakapojengwa.Kushoto aliyesimama ni Meneja wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Tawi la Songea Dkt. Bakari Mashaka.