RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika wakurejesha diplomasia ya Uchumi na kuendeleza biashara baina ya Zanzibar na Comoro kwa maslahi ya pande zote mbili.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 9 Oktoba 2024, Ikulu Zanzibar alipozungumza na Gavana wa Jiji la Moroni, Visiwa vya Ngazija, Bw. Ibrahim Mzee aliyefika na ujumbe wake kuwasilisha dhamira ya kukuza ushirikiano baina nchi mbili hizo.
Aidha Rais Dk. Mwinyi aliushauri ujumbe huo kurejesha makundi ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja Zanzibar kuangalia fursa za biashara na uwekezaji kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Amesema, ni vema kwa pande mbili hizo kufirikia namna ya kurejesha huduma ya usafiri wa vyombo vya baharini ili kuwanufaisha wananchi wa pande mbili hizo na fursa za biasahara na kijamii zilizopo.
Halikadhalika, Dk. Mwinyi alishauri ujumbe huo kuweka utaratibu maalumu kwa walimu wa Zanzibar kwenda Comoro kufundisha Kiswahili au Wakomoro kuja Zanzibar kujifunza lugha hiyo jambo ambalo litakuwa na wepesi kwani lugha za nchini mbili hizi zinashabihiana.
Kwa upande wake, Gavana Ibrahimu Mzee amesifu kasi ya mabadiliko na maendeleo makubwa ya Zanzibar na kusema kuwa nchi yake inakitu cha kujifunza kama ilivyofanikiwa Zanzibar.
Vilevile alimualika Rais Dk. Mwinyi kuzuru visiwa vya Ngazija kwa lengo la kubadilishana uzoefu kwenye nyanja za maendeleo.