Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwa Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua unaogharimu shilingi bilioni 143.2 wakati wa ziara ya kikazi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora tarehe 11 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi na Watendaji mbalimbali mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwa Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua unaogharimu shilingi bilioni 143 wakati wa ziara ya kikazi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora tarehe 11 Oktoba 2024.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza Wizara ya Kilimo pamoja, Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja zinginezo zinazohusika kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi wahusika wote waliofanya ubadhirifu wa shilingi bilioni 1.2 za wakulima wa tumbaku katika chama cha ushirika cha Kisanga wilayani Sikonge.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Sikonge katika mkutano wa hadhara uliyofanyika viwanja vya Tasaf akiwa ziarani mkoani Tabora. Amesema serikali haitoruhusu wakulima kudhulumiwa haki yao hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote waliohusika.
Aidha Makamu wa Rais ameagiza kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria mtuhumiwa mmoja aliyebaki wa utekaji na mauaji ya Afisa Mtendaji wa aliyekuwa katika majukumu yake ya kikazi.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameagiza Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kukarabati miundombinu ya barabara hususani barabara muhimu za kiuchumi za Wilaya ya Sikonge kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Amewasihi wananchi hao kutumia vema siku zilizotolewa za kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwaajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi novemba mwaka huu.
Awali, Makamu wa Rais ameweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwa Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua unaogharimu shilingi bilioni 143.2. Makamu wa Rais amempongeza Balozi wa India hapa nchini Mhe. Bishwadip Dey kwa Taifa la India kufadhili mradi huo mkubwa. Amesema India na Tanzania zimekuwa na urafiki wa muda mrefu na kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu, biashara, teknolojia na maji.
Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea na jitihada za kutatua changamoto za maji kwa vitendo ili kuwainua wananchi kiuchumi na Taifa kwa ujumla. Ameongeza kwamba Wilaya hiyo kwa miaka mingi ilikabiliwa na changamoto ya maji safi na salama hivyo wananchi wanapaswa kutunza miundombinu hiyo ili huduma ya maji iweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesisitiza mradi huo ambao umefikia asilimia 48 kutekelezwa na kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika mapema na mradi huo.