* Waziri Mkuu Majaliwa Asisitiza Maboresho Kitaaluma
*Dkt. Biteko Awashukuru Walimu kwa Mchango Wao
* Dkt. Biteko Aahidi Kuendelea Kushirikiana na Walimu Nchini
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi za Elimu, sekta binafsi na wadau wa sekta ya elimu nchini kuhakikisha walimu wanajengewa mazingira bora ya kazi ili watimize majukumu yao kwa ufanisi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu iliyofanyika leo Oktoba 11,2024 Bukombe mkoani Geita,
Aidha, amewataka kuimarisha programu za mafunzo kwa walimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia huku akiwataka waajiri kuwapa mafunzo walimu pamoja na Taasisi zinazohusika na udhibiti wa ubora waendelee kutimiza majukumu yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini imeendelea kuboresha na kusimamia miundo ya watumishi wakiwemo walimu“ Serikali imeboresha stahiki za msingi za watumishi kwa kupandisha madaraja na kuhakikisha wanapata nyongeza ya mishahara yao kwa wakati,”
Ametaja maboresho mengine “ Serikali imeimarisha miundombinu mahali pa kufanyia kazi ikiwemo kuhakikisha kuna madarasa, mabweni na sasa tumeingia kwenye ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na kuimarisha ajira zao.”
Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 229.9 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya walimu huku akiwataka Maafisa Utumishi kuwasilisha orodha ya walimu wengine wanaohitaji kulipwa nao ili Serikali iweze kuwalipa.
“ Walimu 601,668 nchi nzima wamepandishwa madaraja na Serikali imetumia shilingi trilioni 1.3 kuwalipa. Na niwatake Maafisa Elimu kuwatembelea walimu vijijini na kusikiliza kero zao,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, imeelezwa kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi na Chama Cha Walimu Tanzania ili kujadili masuala ya sekta ya elimu na kuwa Serikali inatambua mchango wao huku ikiwataka walimu kujiendeleza katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya kutumia mtandao kujielimisha.
Akizungumzia tukio la Siku ya Mwalimu Bukombe, Waziri Mkuu amesema tukio hilo linatoa tathimini ya masuala ya elimu wilayani humo na kumpongeza Dkt. Biteko kwa kudhamini na kuendeleza siku hiyo kwa kuwa inaongeza jitihada za viwango vya ufaulu.
Waziri Mkuu amesema katika kuboresha sekta ya elimu na michezo nchini Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inajenga shule 10 za michezo na imeiongezea bajeti Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zaidi ya shilingi bilioni 200 ili kukuza na kuboresha sekta ya michezo nchini.
Pia, Waziri Mkuu ameitaka Mifuko ya Hifadhi za Jamii kuhakikisha walimu wanapata taarifa za michango yao kwa wakati pamoja na pensheni zao wakati wa kustaafu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia amezindua zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura na kutoa wito kwa Watanzania kujitokeza na kujiandikisha katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewashukuru walimu wa Tanzania kwa kuendelea kuheshimisha taaluma yao na kuwa chanzo cha maarifa kwao hakitoki kwingine isipokuwa kwao hivyo wailinde kwa wivu mkubwa taaluma hiyo.
Dkt. Biteko amebainishwa sababu ya Wilaya ya Bukombe kuadhimisha Siku ya Mwalimu ni kuwa mwaka 2015 wakati anachaguliwa kuwa Mbunge, wilaya yake ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya Taifa.
“ Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo mabaya na wao wakaniambia tusiwaache nyuma hivyo tulianza kukutana na kufanya tathimini na sasa tunafanya vizuri,” ameeleza Dkt. Biteko.
Ametaja kuongezeka kwa viwango vya ufaulu kila mwaka “ Katika matokeo ya mwaka jana darasa la saba mkoa tulikuwa nafasi ya pili, darasa la nne tulipata wastani wa asilimia 78 na kuwa nafasi ya pili kimkoa.
Ameendelea Kidato cha pili tulikuwa na ufaulu wa asilimia 98 na mitihani ya kijipima ya Wilaya ya Bukombe tumeshika nafasi ya tatu hivyo niliona tutenge siku moja ya kusema asante mwalimu.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa walimu nchini wasivunjike mioyo waendelee kufanya kazi yao na kuwa maisha yao ni kielelezo cha mafanikio katika Taifa na kuwa wao ni nyota inayoangaza na yeye ataendelea kushirikiana nao.
“ Nataka niwaambie walimu wote nchini Serikali inathamini na kutambua mchango wenu kwa Taifa letu na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi yenu na tayari amepandisha walimu 1,036 wamepandishwa vyeo.” Amebainisha Dkt. Biteko.
Katibu wa Chama Cha Walimu, Tanzania Mkoa wa Geita, Pauline Tinda amesema kuwa tangu mwaka 2019 Wilaya Bukombe imekuwa ikiadhimisha Siku ya Mwalimu ambayo inalenga kutekeleza maelekezo ya UNESCO ya kuwatambua na kutoa tuzo za umahiri kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha masoma ya kusoma kuandika na kuhesabu.
Aidha ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kwa walimu ma ustawi wa walimu kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwapandisha madaraja.
Pia, amemshukuru Dkt. Biteko kwa kudhamini maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani na kuendelea kuthamini mchango wao katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa benki huyo inatambua umuhimu wa walimu nchini na kuwa watu wengi wamefanikiwa kutokana na mchango wao.
“ Sisi tunawapongeza walimu wote nchini. Tumeendelea kuunga jitihada nzuri zinazofanywa ili mwalimu awe na mazingira mazuri ya kufanya kazi. Hadi sasa tumetoa zaidi ya shilingi bilioni 1 ili kununua madawati na leo tunachangia madawati 500 na hii tufafanya ili elimu iwe bora nchini sambamba na kuwa mdau muhimu kwa walimu ikiwemo kuendelea kusikiliza maoni ya walimu nchini,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi wa Jembe Limited, Bw. Dkt. Sebastian Ndege amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika Siku hiyo ya Mwalimu kwa kuwa imekuwa nafasi nzuri kwao kushirikiana na walimu wa Wilaya ya Bukombe.