Kamati ya Ulinzi na Usalama wakitoa heshima kwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete wakati akiingia kwenye Ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani
Baadhi ya viongozi wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye pia alikua ndiye msemaji mkuu kwenye kongamano hilo Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi kutoka vyama sita rafiki na viongozi wa chama na serikali
Na Khadija Kalili Michuzi Tv
KAMANDA wa Jeshi la Zimbabwe Luteni Generali Anselem Nhamo Sanyatwe amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere atabaki kuwa Baba wa Afrika kwa sababu ameweza kuunganisha waafrika kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika harakati za kupigania uhuru wa nchi zilizo katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Luteni Jenerali amesema nchi ya Tanzania imekuwa mfano bora wa kuigwa Barani Afrika kutokana na kuendelea kupokea wageni hasa wakimbizi kutoka katika nchi zao kama Congo, Msumbiji, Burundi, Rwanda, Zimbabwe na nchi zingine kutoka Afrika.
Ameongeza kwa kusema kuwa hivi sasa nchi ya Zimbabwe wameanza kufundisha Lugha ya Kiswahili Mashuleni, Vyuo Vya Elimu ya Juu hivyo kuna baadhi ya Watanzania wamepata fursa ya kufundisha Lugha ya Kiswahili nchini Zimbabwe.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye alikuwa msemaji mkuu wa Kongamano hilo amesema moja ya njia sahihi ya kumuenzi muasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ni kwa kutekeleza kwa vitendo aliyoyafanya wakati wa uhai wake kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali hususani katika Uongozi.
Ameyasema hayo leo 11,Oktoba 2024 wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere chini ya kaulimbiu ‘Mwalimu Nyerere na Vuguvugu la Ukombozi Tafakari Mshikamano, Uongozi, Pan-Africanism na Umoja wa Afrika”, iliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
“Mwalimu alikuwa mtu wa aina hiyo ambaye aliishi maneno yake, Alijitolea maisha yake kwa ajili ya maisha ya watu wachache. Hatuwezi kuzungumza juu ya uhuru na maendeleo katika eneo hili la Afrika bila kumtaja mtu huyu ambaye bado tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwake , na njia pekee ya kumtukuza ni kufanya yale aliyotufundisha wakati wa uhai wake,” amesema Dkt. Kikwete.
Aidha Dkt.Kikwete amesema kuwa imani ambayo nchi nyingine duniani na bara hili wanayo kwa taifa letu ni matokeo ya msingi imara ambao umejengwa chini ya Uongozi wa Mwalimu Nyerere na kuongeza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kulinda na kuenzi mawimbi hayo. .
Amesema kuwa Mwalimu alikuwa mpigania uhuru wa kweli na Mzalendo wa Afrika na ndiye alikuwa Mwafrika wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974.
“Leo, tumekusanyika hapa, watu kutoka nchi mbalimbali kutafakari maisha ya aliyekuwa Kiongozi wetu ambaye aliuthibitishia ulimwengu kwamba binadamu wanaweza kuishi kwa kuheshimiana na kwamba ubaguzi wa rangi, ukoloni mamboleo na aina zote za dhuluma za kijamii zinaweza kupigwa vita tu. ya watu kufanya kazi chini ya umoja na dhamira”, amesema Kikwete.
Dkt. Kikwete amesema kuwa tunachakujifunza kwa Baba wa taifa hasa mzalendo wa kweli aliokuwa nao mwenye kuamini katika misimamo yake ambayo hakukatishwa tamaa wala kuvunjwa moyo katika harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu licha ya kupitia changamoto mbalimbali ikiwemo kushitakiwa, kufikishwa Mahakamani na kuhukumiwa kulipa faini sambamba na kudhihakiwa na wakoloni kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi yetu.
“Nyerere alipitia mambo mengi huku wakimuhoji na kumtaka achague kuendelea na ajira yake ya Ualimu ambayo ilikuwa na mshahara au ataendelea na harakati zake za kupigania Uhuru wa nchi yetu”amesema Dkt.Kikwete.
Akizungumzia umuhimu na sababu za kuanzishwa kwa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Dkt Kikwete amesema kuwa lengo la kuwajengea uwezo wa kada mbalimbali za Uongozi kutoka Vyama sita rafiki ambayo ni CCM, FRELIMO, ANC, ZANU PF, SWAPO na MPLA kwa ushirikiano wa Chama Cha kikomunisti Cha nchini China CPC.
Aidha amewataka Viongozi kuondoa dhana ya kwamba Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ni ya Chama fulani bali ni ya Vyama vyote sita rafiki vya harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Hatahivyo almesisitiza Viongozi ambao wamepewa mamlaka ya kusimamia Shule ya Uongozi kuendelea kuitunza miundombinu ya Shule hiyo na rasilimali zote za Shule zilizopo.
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Prof. Marcellina Chijoriga amesema katika salamu zake za ukaribisho kwamba Kongamano hili limeandaliwa kwa ajili ya kuenzi maisha ya Hayati Mwalimu Nyerere na pia kutumia fursa hiyo kujadili michango yake katika ukombozi wa Bara la Afrika.
Naye Katibu Mstaafu wa NEC Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kanali Rungemela Lubinga amesema elimu ya historia ya harakati za Ukombozi wa Afrika na harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu inahitajika kutolewa kuanzia Elimu ya Msingi, Sekondari na ngazi ya Vyuo Vikuu
Hafla hiyo imehudhuriwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Philip Mangula, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge Ndugu Suo Peng- Naibu Balozi Mdogo na Mwakilishi wa Kikomunisti
Chama cha China na viongozi wengine wengi ikiwamo Mabalozi wa nchi kutoka vyama rafiki.
Luteni Jenerali Ansellm Sanyatwe – Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Zimbabwe, wawakilishi kutoka vyama sita ambavyo ni African National Congress (ANC- Afrika Kusini) SWAPO (Namibia), FRELIMO (Msumbiji), ZANU PF (Zimbabwe), MPLA (Namibia ) na
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwakilishi wa Chama Cha Kikomunisti Cha China (CPC) Mabalozi, Wakuu wa Taasisi za Serikali, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na wakazi wa Kibaha.
Mwalimu Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana amefariki Oktoba 14, 1999 baada ya kuongoza nchi kwa miaka 24.