Na mwandishi wetu,Dodoma.
SERIKALI imefanikiwa kuwekeza zaidi ya shs bilioni 294.96 kwenye miradi 46 ya kimkakati katika Serikali za Mitaa tangu mwaka wa fedha wa 2017/18, huku miradi 26 ikiwa tayari imekamilika, imeelezwa.
Hayo yalisemwa jijini Dodoma leo na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bwana Adolf Ndunguru katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye serikali za mitaa.
Alisema mwongozo huo una lengo la kukabiliana na changamoto za usimamizi duni wa miradi, ukosefu wa utaalamu wa kutosha miongoni mwa watumishi, kuchelewa kukamilika kwa miradi na mingi ya miradi hiyo kutotekelezwa kwa viwango vilivyotarajiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa mwongozo huo ni zana mpya ya marejeleo kwa timu za halmashauri utakaotoa mwongozo hatua kwa hatua wa jinsi ya kuanzisha na kusimamia miradi ya kimkakati ya kuzalisha mapato kwa kutumia makampuni (SPV).
“Mwongozo huu ni suluhisho la changamoto nyingi zinazozikabili halmashauri zetu katika kusimamia miradi ya vitega uchumi katika eneo la utawala, uendeshaji na usimamizi wa fedha.
“Mwongozo huu unaotoa fursa ya mawazo mapya na njia za kibunifu za kuimarisha makusanyo ya fedha, kuimarisha uwezo wa kiufundi wa kusimamia uwekezaji wao wa kimkakati wa kuzalisha mapato na hatimaye kuongeza mapato ya ndani na kuboresha utoaji wa huduma katika ngazi za mitaa, unapaswa kutumiwa na mamlaka zote za serikali za mitaa, ikiwemo bodi za kampuni za kusimamia miradi (SPVs)”, alisema Bw. Ndunguru.
Aidha alisema Serikali inatoa shukurani zake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kwa ushirikiano wao endelevu, msaada wa kitaalamu na kifedha katika kuandaa mwongozo huu pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) juu ya matumizi ya mwongozo huu.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Shirika la UNCDF, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Johnson Nyella, ambaye pia ni Kamishna wa Sera wizarani hapo alisema serikali imekuwa ikigharamia ujenzi na utekelezaji wa miundombinu ya uwekezaji ya kuongeza mapato kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha ikiwemo za miradi ya kimkakati.
“Ni matumaini ya serikali mwongozo huu utaimarisha uwezo wa kitaalamu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika usimamizi wa miradi ya uwekezaji ya kuongeza mapato, hivyo kuongeza uwajibikaji na hatimaye kuboresha utoaji huduma za kijamii katika maeneo yao”, alisema Bw. Nyela.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) nchini, Bw. Peter Malika alisema shirika lao limeweka kipaumbele likishirikiana na serikali katika kusaidia kujenga uwezo na kuwekeza katika maendeleo ya ndani ili kufika malengo yaliyowekwa.
“Mwongozo huu utaweka viwango na kuziwezesha halmashauri na taasisi nyingine za serikali zinazoendesha biashara, kutumia muundo sahihi wa utawala bora ili kuboresha shughuli za miradi, utoaji huduma bora, kuongeza kwa ushiriki wa sekta binafsi na kukuza maendeleo ya ndani ya nchi”, alisema Bw. Malika.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TAMISEMI, Bw. John Cheyo alisema kupitia mwongozo huo wananchi watarajie mafanikio ya miradi ya kimkakati itakayowasaidia kupata huduma bora kama vile afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na nyinginezo.
Hafla ya uzinduzi huo ilitanguliwa na mafunzo ya siku mbili kuhusu matumisi ya mwongozo huu yalitolewa kwa maofisa 72 wa serikali kutoka mikoa tisa na halmashauri 16 yakiongozwa na wakufunzi kutoka UNCDF, TAMISEMI na Wizara ya Fedha. Huku yakihitajika kutolewa kwa halmashauri nyingine ii kuongeza uelewa na kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Kamishna wa Sera akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Johnson Nyella, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika hafla iliyofanyika mjini Dodoma leo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adolf Nduguru (wa pili kushoto), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika hafla iliyofanyika mjini Dodoma leo. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni, Bw. Johnson Nyella, Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji nchini (UNCDF), Bw. Peter Malika na kulia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TAMISEMI, Bw. John Cheyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adolf Nduguru (wa pili kushoto), akiangalia bango linaloonesha mfano wa vitabu vya mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika hafla ya uzinduzi rasmi wa mwongozo huo mjini Dodoma leo. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni, Bw. Johnson Nyella, Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji nchini (UNCDF), Bw. Peter Malika, Naibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Mipango, Dk. Lorah Madete na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TAMISEMI, Bw. John Cheyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adolf Nduguru, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika hafla iliyofanyika mjini Dodoma leo.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) nchini, Bw. Peter Malika, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika hafla iliyofanyika mjini Dodoma leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Bi. Tuse Joune, akizungumza kuridhishwa kwake na juhudi na uamuzi wa serikali katika kuanzisha mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa katika hafla ya uzinduzi wake, mjini Dodoma leo.
Baadhi ya washiriki wakihudhuria uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, mjini Dodoma leo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia uzinduzi wa mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, mjini Dodoma leo.