Jeshi la Polisi Mkoa Arusha limesema kuwa katika baadhi ya vyombo vya habari kumekuwa na taarifa inayosambaa ikisema kwenye nyumba ambayo ulikutwa mwili wa mtoto Mariam Juma aliyeuawa tarehe 12.10.2024 huko kwa Mrombo kumekutwa risiti ambazo watu na baadhi ya vyombo hivyo wanadai ni risiti za malipo ya vifo au mauaji yaliyofanyika kishirikina.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandimizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefuatilia kwa kina na kupata maelezo ya baadhi ya watu na imebainika Baba mwenye nyumba Ramji Hatibu Mlacha, ambaye alikuwa ni mmoja wa viongozi wa chama cha Wapare washio Mkoani Arusha, unaojulikana kama Umoja wa Ushirikiano wa kusafirisha na kuzika Usangi (U.U.K.K), ambapo mmoja wao akipatwa na msiba kuna kiasi cha fedha kila mwanachama anatakiwa kuchanga na anapochanga anaandikiwa risiti nakala hubaki kwa mchangishaji (ambaye ndiyo huyu Baba mwenye nyumba).
SACP Masejo amebainisha kuwa risiti zilizokutwa kwenye nyumba hiyo kwa mujibu wa ushaihidi uliopatikana si risiti za vifo vilivyotokana na ushirikina kama baadhi ya watu na baadhi ya vyombo vya habari vinavyoendelea kupotosha umma.
Sambamba na hilo amesema kuwa nguo mbalimbali ikiwepo masweta imebainika ni vya watoto na wajukuu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo.
Vilevile amesema Jeshi la Polisi Mkoani humo linaendelea kutoa onyo kwa baadhi ya watu wanaoendekeza tabia za kuzusha mambo ya uongo au uzushi bila kuwa na uhakika kutoka mamlaka zinazostahili kutoa ufafanuzi ulio wa kweli.
Kamanda Masejo kemea tabia iliyoonyeshwa na baadhi ya watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kufanya uharibifu katika nyumba ya mtuhumiwa huyo wa mauaji wakati hatua stahiki zilisha huchukuliwa kwa haraka na kwa wakati na Jeshi la Polisi ikiwemo kuwakamata watuhumiwa.
The post Polisi watoa ufafanuzi taarifa inayosambaa kuhusiana risiti za vifo first appeared on Millard Ayo.