Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani Petro Magoti, ametoa tahadhari kwa baadhi ya vijana na akinamama kujiepusha na mikopo ya kibiashara isiyo na nafuu ambayo inafahamika kwa “mikopo ya kausha damu.”
Alisisitiza kuwa mikopo hiyo inaleta mzigo mkubwa wa kifedha kwa wakopaji na kudhalilika .
Alitoa tahadhari hiyo kwenye muendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero za wananchi papo kwa papo katika mkutano wa hadhara ,Kata ya Boga 15, Oktoba 2024.
Magoti aliwahimiza, wananchi kuunda vikundi na kuchukua mikopo kupitia halmashauri, ambapo serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imepeleka fedha kusaidia vikundi vya wananchi.
Vilevile, aliwahimiza wananchi wa Kata ya Boga kutopoteza muda kwenye migogoro ya kisiasa, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, na badala yake wajikite katika kushiriki miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali.
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa Rais Samia ameleta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya Kisarawe, na wananchi wanapaswa kuzitumia kwa ufanisi.
Zaidi ya hayo, Magoti aliendelea kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, akiwakumbusha umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao.