Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
16 Oktoba 2024
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Edson Mwakihaba, ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, ameonya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto vinavyosafirisha abiria na mizigo nyakati za usiku bila kuhakikisha ubora na Usalama.
Amehimiza wamiliki kuzingatia ukaguzi wa kina kabla ya kuvipitisha barabarani.
Mwakihaba alitoa onyo hilo Oktoba 16, wakati wa operesheni maalum ya kukagua makosa ya usalama barabarani, ikiwemo magari mabovu, magari yenye taa moja (chongo), madeni ya serikali, upakiaji wa mizigo hatarishi na ukosefu wa viakisi mwanga pia ni mojawapo ya changamoto kubwa.
Operesheni hiyo ilianza kufuatia uchunguzi uliobaini kuwa magari mabovu pamoja na madereva wasiotii sheria za usalama barabarani usiku ni chanzo kikuu cha ajali na foleni zisizo za lazima.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limejipanga vilivyo kukabiliana na madereva wanaokiuka sheria, hasa nyakati za usiku, ili kuzuia ajali zinazotokana na uzembe huu,” alisema Mwakihaba.
Juma Kassim, dereva wa gari la abiria kutoka Mbezi kwenda Mlandizi, alielezea shukrani zake kwa Jeshi la Polisi kwa operesheni hiyo.
Anasema imemfundisha umuhimu wa kufanya ukaguzi wa kina wa gari lake kabla ya safari ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika kwa kufuata sheria.