Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akifafanua hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wakati akiwasilisha taarifa ya taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa taarifa za taka ngumu na taka hatarishi katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jijini Dodoma leo Oktoba 18, 2024.
………..
Ofisi ya Makamu wa Rais iko mbioni kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa taarifa za taka ngumu na taka hatarishi katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Mfumo huo utasaidia kukusanya taarifa kwa ufanisi, kuchakata maombi ya vibali na kutoa taswira halisi itakayosaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusiana na usimamizi wa taka zinazozalishwa.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alipowasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa mfumo huo wakati wa kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo tarehe 18 Oktba, 2024.
Amesema kuwa mfumo huu utasaidia kubaini sifa, uwezo na vifaa vya kukusanyia na kusafirisha taka vinavyotumiwa na kampuni zilizopewa
kandarasi na halmashauri katika usimamizi wa taka ngumu katika maeneo yao.
Mhe. Khamis amebainisha kuwa kupitia mfumo huu, Serikali itaweza kupata taarifa sahihi za hali ya mazingira, changamoto zilizopo na jitihada zake kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha mfumo wa usimamizi taka nchini na hivyo kulinda mazingira na afya ya jamii.
“Mfumo huu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za usimamizi wa taka ngumu na taka hatarishi nchini. Ni matarajio yetu kuwa, mfumo utasaidia kukuza ufanisi, ufuatiliaji, uwajibikaji pamoja na kuimarisha jitihada za uhifadhi, utunzaji na usimamizi wa mazingira,” amesema.
Ameongeza kuwa Mfumo huo unaoandaliwa chini ya mradi wa Kuimarisha Uwezo waKitaifa wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Maandalizi yake yamefikia 60 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha ujao.
Aidha, Naibu Waziri ametaja hatua zinazofuata ni kuendelea kushirikisha wadau ili kubaini mahitaji mengine yanayohitajika kwenye mfumo ikiwemo Mamlaka ya Serikali (eGA) ili kuukamilisha na kuuboresha kutokana na maendeleo ya teknolojia.
Mfumo utashirikisha watumiaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, halmashauri, wakandarasi na wadau wengine wanaohusika na zoezi za usimamizi, ukusanyaji na usafirishaji wa taka zinazozalishwa.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wake Mhe. Mhandisi Stella Manyanya imeonesha kuridhishwa na uanzishwaji wa mfumo huo.
Aidha, Mhandisi Manyanya pamoja na wajumbe wengine akiwemo Mhe. Prof. Sukurani Manya wamesema upo umuhimu wa kutoa na elimu na kuhamasisha wananchi waweze kutenganisha taka ngumu.