Mbunge wa jimbo la Tarime , Mwita Chacha ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za Gati memorial na Nyahiri akizungumza katika mahafali hayo mkoani Arusha .
Wahitimu wa darasa la saba wakitumbuiza katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Gati Memorial iliyopo mkoani Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Wazazi wametakiwa kutowapangia watoto wao fani za kusoma kwani kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa ya kufanya kile wanachokipenda kwa maisha yao ya baadaye.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa jimbo la Tarime , Mwita Chacha ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za Gati memorial na Nyahiri zilizopo mkoani Arusha wakati akizungumza katika mahafali ya 11 katika.shule ya mchepuo wa kiingireza ya Gati Memorial iliyopo mkoani Arusha .
Amesema kuwa, kumekuwepo kwa changamoto kubwa ambayo inalalamikiwa na watoto walio wengi kuhusu wazazi kuwapangia fani za kusoma jambo ambalo linawakatisha tamaa ya kufikia ndoto zao.
“Kila mtoto ana malengo yake ya kuwa mtu fulani katika maisha yake ya baadaye hivyo wanavyosoma wana matarajio yao sasa mnapowapangia tena kozi ya kusoma mnakatiza ndoto zao za baadaye kwa kusomea fani wasizozipenda jambo ambalo linawakatisha tamaa sana .”amesema Mwita .
Aidha amefafanua zaidi kuwa,wapo wahitimu wengi ambao wamehitimu vyuo vikuu na wamesomea kazi ambazo hazikuwa chaguo lao imewabidi wasome tu kutokana na kushinikizwa na wazazi wao ila sio kwa kupenda wao wenyewe.
Amefafanua zaidi kuwa,ni lazima wazazi wawape nafasi watoto wao wachague kile moyo wao unataka na sio wazazi kuwachagulia maana mwisho wa siku inasababisha kuwa na wataalamu wasioipenda kazi yao .
“Ili tuweze kupata wataalamu wenye moyo zaidi tuwaache tu wasomee kile wanachokipenda kuliko kuwachagulia fani ambazo haziendani na wanachohitaji wao.”amesema Chacha.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Beatha Shirima amesema kuwa wamekuwa wakiwajengea watoto mazingira ya kuweza kujitegemea wenyewe na kuweza kuwa viongozi wa kesho.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuendelea kuendeleza nidhamu ya watoto hao ambayo walikuwa nayo tangu wakiwa shuleni ili waendelee kuitangaza shule hiyo.
Kwa upande wa wanafunzi katika.mahafali hayo ,wameipongeza shule hiyo kwa namna ambavyo imekuwa ikiwaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye kwa kuwafundisha namna ya kuweza kujiamini na kuwa viongozi bora wa kesho pamoja na kufundishwa masomo ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wao wenyewe.