Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amesema mabadiliko ya kweli kwenye jamii yanaanza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kujiandikisha kwenye daftari la mkazi kisha kupiga kura kuchagua Viongozi bora na wazalendo ifikapo Novemba 27 mwaka huu 2024.
DC Kasilda ameeleza hayo akiwa Kata ya Hedaru kwenye mbio za hiari (Jogging) maalum kuhamasisha ushiriki wa wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mkazi lililo anza Oktoba 11 na kutarajiwa kutamatika Oktoba 20, ambapo zoezi hilo humwezesha mwananchi kuwa na sifa za kushiriki kupiga kura Novemba 27 kuchagua Viongozi wa Mtaa/Kitongoji chake.
“Kichinjio tarehe 27 huwezi kukipata kama hutajiandikisha hizi siku mbili zilizobaki, lakini naomba niwaambie lazima mchague Viongozi bora na siyo bora viongozi, chagueni Viongozi ambao watabeba shida zenu”. Alisema DC Kasilda.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same Abdallah Mnyambo amesema kinachoendelea kwenye maeneo mbalimbali nchi ya Tanzania kwa sasa ikiwemo Wilaya ya Same (zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa) ni mchakato wa kidemokrasia unaowezesha kupata Viongozi watakao wawakirisha wananchi kusukuma gurudumu la maendeleo hivyo ni vyema wananchi wakajitokeza kushiriki ipasavyo kwenye mazoezi yote yanayoendelea.
Naye Yohana Peter Afisa Uchaguzi Wilaya hiyo amesema Serikali ilitoa siku kumi (10) za uandikishaji wananchi kwenye daftari la mkazi kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu 2024, hivyo ni wakati sasa umefika kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa.