*Kamisaa wa Sensa asema ripoti inasubiliwa na wananchi.
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
OFISI ya Taifa ya Takwimu(NBS) imesema kuwa wananchi wanasubiri ripoti ya kina kwa ajili ya kutumia katika maendeleo ambapo ifikapo Desemba 02, mwaka huu rasimu zote za ripoti za takwimu za sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 zitakuwa zimekamilika.
Hayo ameyasema jijini Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Salum Kassim Ali kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali , Dk Albina Chuwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha uandishi wa ripoti za kina zitokanazo na matokeo ya sensa ya watu na makazi mwaka 2022.
Amesema ya ripoti za kina zitokanazo na matokeo ya sensa ya watu na makazi mwaka 2022 na kuongeza kuwa kuzinduliwa rasmi awamu hii ya kwanza ya Uandishi wa Ripoti za Kina kunatokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Kutokana na miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu ufanyaji wa Sensa ya Watu na Makazi, zoezi hili hukamilika tu pale ambapo uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa zimechakatwa, zimechambuliwa na kuandaa ripoti za aina mbalimbali na ripoti hizo zitumike kikamilifu katika kufanya maamuzi mbalimbali yenye tija kuhusu mendeleo endelevu ya watu na makazi.
“Kwa msingi Serikali inaendelea na utekelezaji wa Awamu ya Tatu na ya mwisho ya zoezi la Sensa, katika awamu hii, Serikali imefanikisha kuandaa ripoti zote 24 za msingi ambazo zimeshazinduliwa rasmi,”amesema
Ali amesema serikali imeendelea kusambaza na kufanya mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa kwa viongozi na watendaji katika ngazi mbalimbali za utawala.
Ripoti ambazo zimeshakamilika zimebainisha viashiria vya msingi kwa jumla wake katika maeneo ya mgawanyo wa idadi ya watu katika ngazi mbalimbali za kiutawala, umri na jinsi, majimbo ya uchaguzi, takwimu za msingi za kidemografia, kijamii, kiuchumi na mazingira pamoja na takwimu za msingi za Sensa ya majengo.
Amesema Kitaalamu, ripoti hizo ni lazima ziandaliwe kwa kutoa picha ya hali ilivyo, maeneo yenye
changamoto na fursa zilizopo kuiwezesha Serikali na wadau wengine kubuni na kutekeleza afua za kimakakati za kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na thibiti wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi wake.
“Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha wadau wetu wote kuwa, rasimu za ripoti 31 za takwimu za msingi za kidemografia, kijamii, kiuchumi na mazingira kwa mikoa yote nchini na ripoti ya Makadirio ya Idadi ya Watu kuanzia mwaka 2023 hadi 2050 zimekamilika.
Ali amesema rpoti hizi zitazindulia rasmi hivi karibuni kwa ajili ya matumizi kwa Umma.
Amesema baada ya kukamilisha uandishi wa ripoti za msingi za Sensa, Serikali imeelekeza nguvu zaidi katika uandishi
wa ripoti za kina za kisekta ambazo zimejikita katika kufanya chambuzi wa kina katika maeneo mahsusi.
Ali amesema maeneo yanayofanyiwa uchambuzi wa kina ni kati ya maeneo ya vipaumbe vya nchi ambayo yanahitaji takwimu za kina kufanya maamuzi sahihi zaidi ya kukuza na kuimarisha maendeleo ya watu.
Hata hivyo serikali imepanga kuandaa ripoti 15 za kina ambapo kazi hii itafanyika kwa awamu mbili.
“Katika awamu hii ya kwanza ambayo ndio imetukutanisha hapa leo, zitaandaliwa ripoti tano za kina katika maeneo ya Vizazi na Ndoa, Vifo na Afya , Hali ya Ulemavu, mienendo ya Idadi ya Watu na Elimu na kujua kusoma na kuandika.
Amesema lengo la kuandika ripoti hizi za kina za matokeo ya Sensa kama inavyopendekezwa na Umoja wa Mataifa ni kupata uelewa mpana zaidi wa hali ilivyo katika maeneo mahususi katika Nchi, kubaini mienendo, changamoto na fursa zilizopo kuwezesha viongozi na watendaji kuhuisha sera na mipango ya maendeleo inayoakisi hali halisi ya mahitaji ya wananchi.
Ripoti ya kina ya Mienendo ya Idadi ya Watu itawezesha kubaini mienendo ya idadi ya watu kwa umri na jinsi kati kipindi kimoja na kingine kwa kulinganisha na ukuaji wa uchumi na viashiria vingine kama vile hali ya uhifadhi wa mazingira na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa ajili ya kuweka mikakati ya makusudi ya kuboresha maisha ya watu wote.
“Napenda kukuhakikishia kuwa tunao utaalamu wa kutosha ndani ya Nchi yetu kwa ajili ya kuifanya kazi hii muhimu ya kitaifa. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshghulikiwa Idadi ya Watu hapa Nchini, limeingia mkataba na Profesa Akim Mturi ambaye ni Mtanzania kuwa, awe Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kitaalamu katika kufanikisha kazi hii,” amesema.
Alisema kazi hiyo ni kubwa na inahitaji utulivu, umakini, moyo wa kuijituma, kujitolea na uzalendo wa hali ya juu hivyo itatumia siku 14 kuchakata na kuandika rasimu za ripoti hizo.
Aidha, rasimu hizo zitawasilishwa katika Kamati za Sensa ngazi ya Taifa kwa ajili ya kuridhiwa uzinduzi wake.
Amesema Dkt.Albina aliagiza kazi hiyo ipewe nafasi ya kipekee katika kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa kwa kuwa inasubiriwa na Serikali na wadau kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kimkakati yanayohusu maendeleo ya wananchi katika maeneo husika.
“Uandishi wa ripoti hizi za kina ni tofauti kidogo na ripoti zilizopita, hivyo natoa wito mzingatie yale yote ambayo Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kitaalamu atakuwa anawaelekeza ili kufikia malengo liyojiwekea,” alisema.
Kea upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika Mstaafu, Anne Makinda aliwataka kitumia utaalamu walionao kufanikisha kazi wanayoifanya ya uamdishi wa ripoti kwa viwango vya ubora na uwezo huo wanao.
“Ninazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia takwimu za sensa kufanya maendeleo ya watu kwani kuendelea kuimarisha taarifa kunaipa tahamani uwekezaji unaofanywa na awrikali kushirikiana na wadau wa maendeleo, ” amesema
Kamisaa wa Sensa,Spika Mstaafu Anna Makinda akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uandishi wa Ripoti ya Sensa na Makazi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Balozi Mohamed Haji Hamza akizungumza kuhusiana na kazi walionao wachambuzi wa uandishi wa ripoti matokeo ya Kina wakati uzinduzi wa mafunzo ya Wataalam jijini Dar es Salaam.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salum Kassim Ali akizungumza kuhusiana na mafunzo kwa waandishi wa ripoti ya matokeo ya Sensa kwa Kina ,jijini Dar es Salaam.
Mshauri wa Uandishi wa Ripoti ya Matokeo Sensa kwa Kina Profesa Akim Mtulia akizungumza walivyojizatiti katika kufanya kazi hiyo ,jijini Dar es Salaam.
Kamisaa wa Sensa,Spika wa Bunge Mstaafu Anna Makinda akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa kuandaa ripoti ya Kina ya Matokeo ya Sensa mara baada ya kuzinduliwa,jijjni Dar es Salaam.