Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za kiuchunguzi linaendelea na uchunguzi wa matukio matatu yaliyotokea maeneo tofauti Oktoba 19,2024.
Tukio la kwanza ni la wizi wa vitabu viwili vya zoezi la kuandikisha wapiga kura lililotokea Oktoba 19,2024 majira ya saa nane usiku huko Kikelelwa Tarakea Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Tukio la pili ni la Kujaribu kuchoma moto Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Kikelelwa Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro. Uchunguzi huo unakwenda sambamba na kuwafuatilia wahusika waliopanga na kutenda uhalifu huo ambapo hadi sasa watu wanne wanashikiliwa.
Aidha, Jeshi la Polisi lilifuatilia kwa karibu njama zilizopangwa na Chama kimoja cha Siasa za kuvamia na kupora vitabu vya kuandikisha wapiga kura kwa madhumuni wanayoyajua wao wenyewe. Tunatoa tahadhari kwa waliokaa na kupanga uhalifu huo kuwa ni kosa kisheria lakini wasithubutu kutekeleza njama hizo kwani hatua kali kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa dhidi yao.
Jeshi la Polisi lingependa kuwahakikishia wananchi kuwa limejipanga vizuri kuhakikisha uandikishaji unakamilishwa vizuri leo na ambao hawajajiandikisha wasisite kujitokeza kujiandikisha bila hofu yeyote ile.
Pia Jeshi la Polisi baada ya kupokea taarifa ya kuokotwa porini Aisha Machano huko Kibiti uchunguzi umeanza mara moja kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Hivyo tunatoa wito kwa wananchi watulie, uchunguzi utatoa majibu sahihi ya nini kilichotokea dhidi yake, sababu zake ni zipi, wahusika ni nani na hatua zitachukuliwa kulingana na ushahidi utakao patikana kwa mujibu wa sheria.
David A. Misime DCP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma,Tanzania