Mkuu wa Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Botswana (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda ameongoza kikao cha Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama ya SADC TROIKA kupitia taarifa ya maandalizi ya Misheni hiyo nchini Botswana.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 20 Oktoba 2024 na kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Organ; Malawi Mwenyekiti ajaye na Zambia ambayo ni Mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Sekretarieti ya SADC.
Kikao kimepokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa na Sekretarieti ya SADC kuhusu maandalizi ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Botswana utakaofanyika tarehe 30 Oktoba,2024.
Sekretarieti pia iliwasilisha mgawanyo wa majukumu kwa timu mbalimbali za misheni hiyo katika uchaguzi huo.
Katika kikao hicho Mhe. Pinda amesema ni matumaini yake kuwa maandalizi na Mipango ya Uangalizi itaenda sawa na hivyo kuifanya SEOM kutekeleza jukumu lake kwa tija na ufanisi.
Amesema pia SEOM ıkifanya kazi yake ya uangalizi na kuandaa taarifa za Uangalizi wa uchaguzi huo itasaidia nchi husika kufanya maboresho katika mifumo yake ya demokrasia na hivyo kuwa sehemu ya kukuza demokrasia katika nchi wanachama.